Kiswahili 34. “Upendo wa Mwenyezi Mungu…katika kusamehe dhambi”

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!
Salamu katika jina la Mwenyezi Mungu atupendaye sisi kwa upendo wa milele. Mpendwa msomaji, Wakristo wengi ambao hawajui wanasema kwamba Mwenyezi Mungu katika Kurani hana upendo, au kwamba kwa shida sana upendo unatajwa katika Uislamu.
Lakini twaikuta aya ya maana sana katika Sura 3:31 Aali Imran

 

“…Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakughufirieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira (na) Mwenye Rehema.”

Mimi, kama Mwadventista Msabato, nagundua ya kwamba upendo umetajwa zaidi ya mara hamsini katika Kurani Tukufu na ya kwamba neno hili ‘msamaha’ na maneno yenye maana inayokaribiana sana yatokanayo na neno lilo hilo yanapatikana humo zaidi ya mara mia mbili! Je, msamaha si kipengele dhahiri cha upendo? Kusema machache tu hilo ni jambo la kushangaza. Somo ninalotaka tulipitie leo ni jinsi upendo wake Mwenyezi Mungu unavyodhihirishwa katika kusamehe dhambi.

Kama tusingekuwa na msamaha wo wote kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tungekuwa tumepotea milele. Kurudi mbali kule nyuma katika siku zile za Adamu alipokuwa Peponi, alifanya dhambi na kupoteza njia yake. Kwa vile sisi tu watoto wake Adamu, sisi pia tulipoteza njia na kwa sababu ya dhambi yake sisi tumerithi tabia isiyokuwa na upendo wa kweli na twaweza kutarajia tu mauti ya milele.

“Kwa hiyo kama kwa mtu mmoja [Adamu] dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.” Injili Warumi 5:12

Walakini, huo si mwisho, Kurani Tukufu inasema “nitawafutia makosa yao.” Sura 3:195 Aali Imran, pamoja na “msamaha mzuri” wa Mwenyezi Mungu. Sura 15:85 Al Hijr. Lakini ni kwa vipi hilo linatekelezwa kwa mwanadamu? Kipeperushi hiki kidogo kitaichunguza kweli hii ya zamani kwa njia mpya mbalimbali.

Kwa ajili ya ahadi hizi sisi tunalo tumaini tuwezalo kulishikilia ambalo wale wasioamini hawanalo. Tungejihesabu wenyewe kuwa tumebarikiwa kuifanya habari hii ijulikane kwa wote wanaotuzunguka. Kurani Tukufu yatuambia sisi kwamba:
“…Tuliwafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine (kwa amali zao zilizo bora zaidi kuliko za wenziwao), na Daudi tulimpa Zaburi.” Sura 17:55 Bani Israeli

Katika Zaburi twasoma: “Lakini kwako kuna msamaha, ili Wewe uogopwe.” Zaburi 130:4. Daudi pia alisihi: “Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu, uzifute hatia zangu zote.” Zaburi 51:9

Gharama ya Msamaha!

Kwa wengi, mawazo kidogo tu huelekezwa kwenye gharama aliyolipa Mwenyezi Mungu kwa kutupa sisi msamaha kwa ajili ya dhambi zetu. Kumbuka kwamba mtu anapofanya dhambi na kutenda tendo baya, daima kuna gharama au malipo.

Mtu fulani anapokukosea wewe, kwa mfano, ameiba kitu fulani cha thamani kutoka nyumbani mwako, kama vile Televisheni yenye skrini kubwa, kisha mwizi huyo anakamatwa, mambo kadhaa yaweza kutokea.

Mwizi huyo aweza kusamehewa, kisha wewe unabeba hasara ya Televisheni yako yenye skrini kubwa! Hivyo wewe unapata hasara.
Mwizi huyo aweza kufungwa gerezani, kisha yeye anateseka kwa kupoteza uhuru wake.
Mtu fulani mwingine, kwa wema wa moyo wake, anajitolea kukupa Televisheni badala ya ile ya kwako. Mwizi anaenda zake akiwa huru. Mtu mwingine huyo anapata hasara mwenyewe.

Kumbuka ya kwamba sikuzote msamaha huja na gharama yake, sikuzote mtu fulani analipa. Hilo linapokuja kwenye dhambi zetu, twaweza kuingia gharama na kulipa bei kwa ajili ya dhambi yetu na kupoteza uzima wa milele kama mshahara wake. “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti…” Warumi 6:23

Kesi hiyo ya tatu ndivyo alivyotufanyia sisi Mwenyezi Mungu. Kama tungeteseka kwa ajili ya dhambi zetu, basi, tungepoteza uzima wetu milele, lakini kwa sababu ya upendo wake Mwenyezi Mungu, yaani, wema wake na rehema zake kwetu, kwa hiari yake amechukua kesi hiyo mwenyewe. Amemtoa mtu mmoja aliyekuwa kifuani pake Mwenyezi Mungu ili alipe gharama ya dhambi zetu. Ametoa uhai wa Mwanawe pekee badala ya ule wetu. Alikuwa ni yule mtu mmoja aliyekuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu. Aliitwa Neno la Mwenyezi Mungu, Kalimatu wa Mwenyezi Mungu. Sura 3:39; 3:45; 4:171.
“(Kumbukeni) waliposema malaika: ‘Ewe Maryamu! Mwenyezi Mungu anakupa khabari njema za (kumzaa mtoto bila ya mume, bali kwa kutamkwa Neno tu litokalo kwake (la kukwambia ‘Zaa’ ukazaa pasina kuingiliwa). Jina lake ni Masihi Isa, mwana wa Maryamu, mwenye heshima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa waliopelekwa mbele na Mwenyezi Mungu.” Sura 3:45 Aali Imran
Mwenyezi Mungu alionesha pendo lake kwetu sisi … “alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Warumi 5:8

Ndiyo, rafiki zangu wapendwa, jambo hili mara nyingi hatulitilii maanani! Mtu fulani alilazimika kulipa bei kwa ajili ya dhambi yetu! Gharama ya msamaha ilikuwa kubwa, kubwa mno, yaani, mauti!

“Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.” Injili Warumi 5:10

“Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.” Injili Matendo 5:30-31

Kwa hiyo gharama ya msamaha wetu ilikuwa mauti … mauti ya Masihi Isa. Kwa njia hii haki ilitimizwa na rehema iliifikia familia ya mwanadamu. Mwanadamu angeweza kwenda zake akiwa huru kwa sharti kwamba atii masharti ya ukombozi. Mwanadamu anahitaji kuamini na kupokea kile alichofanya Mwenyezi Mungu.

“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Injili Waefeso 1:7

Msamaha Waoneshwa Wazi!

Masihi Isa alikuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu na kwa wazi kabisa Isa alimwakilisha Mwenyezi Mungu kiasi kwamba yeye asema:
“ Aliyeniona Mimi amemwona Baba.”
Injili Yohana 14:9
Twapata picha nzuri zaidi ya msamaha wake Mwenyezi Mungu tuonapo jinsi Isa alivyowatendea wale waliomtesa walipokuwa wakimsulibisha msalabani ili auawe. Hapo twaona msamaha wenye kina ukioneshwa katika maisha yake Isa na kwa kiwango kikubwa mno kisichowahi kuonekana duniani kabla ya hapo. Kumbuka kwamba Isa ni “chapa ya nafsi yake” Mwenyezi Mungu. Hapa ipo aya iliyo wazi inayoelezea ukaribu wake kwa Mwenyezi Mungu.

“Yeye [Mwana] kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu…” Injili Waebrania 1:3

Askari wale wa Kiroma walipompigilia Isa kwa misumari pale msalabani kutokana na ombi la Wayahudi … ulionekana tu upendo mwingi na unyenyekevu katika moyo wake Isa. Hakuna chuki aliyoionesha na wakati walipokuwa wakifanya kazi ile ya kuogofya, Isa alikuwa akiwaombea, akisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Na wale askari wakayapigia kura mavazi yake. Injili Luka 23:34
Sala ile ya Isa ya msamaha iliujumuisha ulimwengu mzima. Kwa wote msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia Isa unatolewa bure. Ye yote atakaye aweza kuwa na amani kwa Mungu na kurithi uzima wa milele. Hakuna kisasi cho chote kilichotamkwa juu ya wale askari, makuhani, au watawala, Isa aliwahurumia kwa ujinga wao na hatia yao. Alitoa tu lile ombi ili wapate msamaha wao.

Wapendwa rafiki zangu, mwaweza kufanya uwezekano uwepo ili sala ile ya Masihi Isa ipate kujibiwa katika maisha yenu. Sala ile inamjumuisha kila mtu aliyewahi kuishi, ilimjumuisha kila mtu kutoka katika familia nzima ya Adamu.
Ni Mwenyezi Mungu aliyemteremsha Isa humu duniani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na athari yake. Isa alijipatia haki ya kutusamehe na sasa sisi tunasimama katika upendeleo huo mtakatifu wa kurejeshwa mara moja tena Peponi mwa Mungu. Ni upendo na msamaha wa ajabu huo!

Gharama Kubwa ya Msamaha!

Wengine huenda waweza kuonekana kana kwamba wanafikiri lilikuwa jambo dogo tu kwa Baba kumteremsha Isa duniani kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu.

Ingawa mpango wa wokovu ulikuwa umewekwa muda mrefu kabla ya uumbaji wa dunia hii;… bado lilikuwa ni pambano hata kwa yule Mfalme wa malimwengu kumtoa Mwanawe pekee ili afe kwa ajili ya jamii yenye dhambi. Lo, siri ya ukombozi hiyo! Upendo wa Mungu huo kwa ulimwengu ambao haukumpenda! Katika vipindi visivyo na mwisho, akili za wale wasiokufa, wakitafuta kuifahamu siri ya upendo huo usioweza kufahamika, watashangaa na kumsujudu.

Basi, sisi twaweza kuitikia kwa njia ya toba kwa Mungu na imani kwa Kristo. Hivyo ndivyo wana wa Adamu walioanguka wawezavyo tena kuwa “wana wa Mungu” wa kupanga.

Injili 1 Yohana 3:1-3
“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu, na ndivyo tulivyo. Sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.”
Mpendwa, rafiki yake Mwenyezi Mungu, leo hii wewe waweza kufanya maamuzi yako kukubali na kuamini ya kuwa Masihi Isa ndiye yule Mmoja aliyeteremshwa katika dunia hii yenye giza kulipa fidia yetu kwa kutoa uhai wake na damu yake. Kukataa toleo hilo la gharama kungekuwa ni tusi dhahiri kwa Mwenyezi Mungu kwa msamaha wake kwako wewe. Leo hii, uweze kuchagua kuwa na amani kupitia kafara hii ya Masihi Isa!

Kwa maelezo zaidi tafadhali ujisikie huru kuwasiliana nasi kwa tovuti hii chini:
www.salahallah.com

“Upendo wa Mwenyezi Mungu…katika kusamehe dhambi”

Sura 3:31
Aali Imran

Mfululizo na.34