Kiswahili 26. Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu… moyo wako!

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalaamu Aleikum

 

Pokea salamu zangu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema nyingi sana na Mwenye Huruma nyingi sana na ambaye huwahurumia wanaopotea. Amani tamu ya Mwenyezi Mungu na iwe pamoja nawe leo. Naomba uwe na ujuzi wa Neno lake pamoja na kuwa na Neno lake ndani yako!

Mfalme wa kidunia ana mamlaka, kiti cha enzi na raia wa ufalme wake. Lakini ni vipi kuhusu Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu? Mpaka wapi kinafika hicho Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu? Kurani Tukufu yatoa jibu kwetu…
‘Enzi yake imeenea mbingu; na ardhi; …Yeye (peke yake) ndiye aliye juu na ndiye aliye Mkuu.’ Sura 2:255 Al-Baqarah

Katika Zaburi nabii Daudi anatuambia sisi…
“BWANA ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake unavitawala vitu vyote.”
Zaburi 103:19

Ni wazi yaonesha kwamba mamlaka yake Mwenyezi Mungu inaenea juu ya ulimwengu wote ulioumbwa. Hata hivyo kuna mahali pamoja asipoweza kutawala, katika mapana yote ya ulimwengu bado kuna mahali pamoja ambapo hawezi kusimika bendera yake. Lakini, je, miliki hiyo i wapi? Si nyingine zaidi ya ule moyo wa kibinadamu ambao hautaki.

Taurati yatuambia tena kwamba “moyo [wa kibinadamu] huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” Yeremia 17:9
Moyo wa kibinadamu ambao haujafanywa kuwa mpya hauna mahali pa kukaa Mwenyezi Mungu, kwa maana utawala wake kwa hao ni mgeni.
Chaguo ni letu!
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu hatumii nguvu kuingia ndani ya mtu ye yote, basi, sisi tunao uhuru wa kuchagua nani atakuwa Bwana wetu. Mabavu hayatumiki katika Ufalme wa Mwenyezi Mungu, je, wakumbuka aliyosema Isa (Yesu) kuhusu ufalme wake?
‘Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.’ Injili ya Yohana 18:36

Angalia kwa makini maneno haya kutoka katika Kurani Tukufu.
Sura 2:256 “Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika dini: Uongofu umekwisha pambanuka na Upotofu: basi anayemkataa shetani na akamwamini Mwenyezi Mungu, bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika.”

Ufalme wake Mwenyezi Mungu hauhitaji mkono wo wote wa kibinadamu kutumia nguvu kuwalazimisha raia zake. Wale wanaokuwa raia wa ufalme huu hufanya hivyo kwa hiari, bila ya kutumika nguvu yo yote kutoka nje.

Hoja tunayotoa leo ni hii, Je, ni nani anayetawala juu ya kiti cha enzi cha moyo wako? Je, Mwenyezi Mungu yupo pale, au ni nafsi [yako] inayojipenda yenyewe iliyoketi juu ya kiti hicho cha enzi? Hii ni hoja adilifu ambayo kila mmoja wetu angepaswa kujiuliza mwenyewe mara kwa mara. Hivi ni nani hasa anayetawala maisha yangu. Je, ni Mwenyezi Mungu anayetawala au ni mimi?

Mara nyingi wale walio katika familia ya mtu wanaweza kueleza wewe ni mtu wa aina gani wanapoishi nawe. Je, wewe u mpole tena una huruma? Je, unahamaki mara kwa mara, unawakasirikia watoto na kutupa vitu huku na huku kwa ghadhabu? Au unayo amani thabiti moyoni mwako? Ni maneno gani usemayo kila siku? Je, ni maneno makali, au ni ya amani na yenye kusaidia. Je, ni roho gani inayoutawala moyo wako?
Je, hivi moyo waweza kugeuzwa?
Naam, lakini si kwa uwezo wake wenyewe. Kupata badiliko katika moyo wa kibinadamu kwahitaji kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu. Ni yeye peke yake awezaye kuugeuza moyo wa kibinadamu ulio mwovu na kuufanya uwe mpole na wenye upendo.

“Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”
Taurati Yeremia 13:23
Tukijaribu kama tutakavyo kwa kutumia juhudi zetu za kibinadamu mbali na Mwenyezi Mungu, hatuwezi kuigeuza mioyo yetu wala kutafuta njia ya kwenda mbinguni kwa kufanya matendo yetu mema.

Lakini Mwenyezi Mungu bado anashughulika kufanya miujiza, na inachukua mwujiza kuugeuza moyo wa kibinadamu. Ili hilo lifanyike ni lazima tujisalimishe. Twahitaji kumpa Mwenyezi Mungu ruhusa ili apate kutawala ndani ya mioyo yetu.

Tangu lile anguko la Adamu katika bustani ile ya raha kuu, mioyo yetu na mawazo yetu yamechafuliwa na kujaa hadaa, wala hatuwezi kuyatumainia. Ibilisi ameipotosha mioyo yetu kwa maovu na dhambi. Lakini ye yote anayependa kumgeukia Mwenyezi Mungu, moyo wake unaweza kufanywa mpya.

Je, ni kwa njia gani moyo wa kibinadamu hugeuzwa?
Katika Taurati tunaelezwa wazi kwamba moyo wa kibinadamu ni mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?
Yeremia 17:9
Lakini bado tunayo ahadi katika Injili inayosema juu ya wale walio heri ambao ni “wenye mioyo safi” maana “hao watamwona Mungu”. Injili ya Mathayo 5:8.

Ni zaidi ya vile inavyoeleweka ya kwamba badiliko lazima litokee kabla moyo wa kibinadamu haujaweza kuwa safi na makusudi ya moyo kuwa maadilifu! Mwenyezi Mungu aliandaa njia ya kutimiza hayo.

Miaka mingi iliyopita Mwenyezi Mungu alimtuma mmoja aliyefanana naye kitabia. Ndiye Yule aliyeteremshwa…tangu milele zote Isa Masihi (Kristo) alikuwa umoja na Mungu, na wakati alipotwaa asili ya kibinadamu, bado yeye aliendelea kuwa umoja na Mungu. Yeye ndiye kiungo muhimu kinachomwunganisha Mwenyezi Mungu na binadamu. “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye [Isa Masihi] naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo,” Injili (Waebrania 2:14). Ni kwa njia ya Isa Masihi tu sisi tunaweza kuwa watoto wa Mungu. Kwa wale wote wamwaminio, anawapa uwezo wa kuwa wana wa Mwenyezi Mungu. Hivyo kwa njia ya ‘kiungo’ hiki, yaani, Isa Masihi, moyo wa kibinadamu unageuka na kuwa hekalu la Mungu aliye hai. Ni kwa sababu Kristo alitwaa mwili wa kibinadamu ndiyo maana wanaume na wanawake wanashiriki tabia yake ya uungu. Yeye ndiye aletaye uzima na hali ya kutokufa kwa njia ya injili. Hivyo kwa kumpokea Yeye (Isa) ambaye aliteremshwa, kwa kukipokea kipawa hiki, badiliko kamili linatokea mioyoni mwetu na Mwenyezi Mungu anatawala juu ya kiti cha enzi cha moyo wa kibinadamu. Maisha yetu yote hubadilika, kutoka yale ya kutenda dhambi kwenda yale ya kutaka kutenda matendo mema na kutenda wema usio na ubinafsi kwa wote watuzungukao.

Mpendwa rafiki, je unatamani Mwenyezi Mungu aketi juu ya kiti cha enzi cha moyo wako? Je, unataka kuacha kabisa matendo maovu na ya dhambi unayotenda katika maisha yako? Je, unataka mawazo yako machafu yasitawale maisha yako tena? Naam, hayo yote yanaweza kufanyika, leo hii mpokee Kristo mchukuzi wa dhambi [al-fida] ndani ya moyo wako. Mwombe Isa Masihi aingie moyoni mwako na kukupa maisha mapya, maisha mapya ndani ya Kristo.

Miaka mingi iliyopita, Israeli ya kale ilimchagua bwana mwingine, waligeuka na kwenda mbali na Mwenyezi Mungu na kumchagua Ibilisi [Shetani] badala ya Mwenyezi Mungu.
Bwana ananena kwa nguvu, akisema, “Haya ndiyo maangamizo yako, Ee Israeli.” “Sikia, Ee nchi; nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa.” Taurati Hosea 13:9; Yeremia 6:19.

Isa anataka kurejesha amani ndani ya mioyo yetu inayosumbuka. Isa ndiye yule Mmoja atakayeleta dhamiri mpya ndani ya maisha yetu. Hapo ndipo tutatafuta kuwa safi na kuwa na tabia yenye upendo. Moyo huu mpya unakuja kama matokeo ya kuyakabidhi maisha yetu kwa Isa Masihi aliyeteremshwa kwetu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii mpendwa rafiki usiruhusu kitu cho chote kukuzuia kupokea kipawa hiki cha thamani kitokacho Mbinguni. Onja na kuona kama Mungu hatakubariki wewe kupitia Isa Masihi aliyeteremshwa kwa ajili yako!
Hivi mimi naanzaje?
Tafuta mahali palipo kimya, ambapo huwezi kuvurugwa. Kisha toa dua yako binafsi kwa Mwenyezi Mungu ukimwomba kupitia kwa Isa Masihi ili ajidhihirishe Mwenyewe kwako kwa njia ya pekee. Mwombe akupe amani na moyo mpya, mawazo mapya na matendo mapya. Mwombe atawale katika kiti cha enzi cha moyo wako. Mwenyezi Mungu anapenda kujibu sala ya imani kama hiyo.
Baadhi ya watu wanaweza kuuliza, Lakini mimi naogopa, je, nifanye nini? Mara kwa mara katika Vitabu Vitakatifu [Taurati na Injili], Mwenyezi Mungu alipomtuma malaika kwa wale waliokuwa duniani, maneno ya kwanza yaliyonenwa yalikuwa “usiogope” au “usiwe na hofu”. Mwenyezi Mungu atakuongoza kama utapenda kuongozwa na kuingizwa katika kweli.
Mpendwa rafiki wa Mwenyezi Mungu. leo mkaribishe awe rafiki yako wa karibu sana kuliko ulivyopata kumjua kabla. Yeye anatamani sana kuwa rafiki yako, tena anatamani sana kumdhihirisha kwako huyo Isa Masihi, ambaye ni sadaka kwa ajili ya dhambi. Ionje amani yake leo.

Mwenyezi Mungu na akubariki sana na kukupa faraja katika siku hizi ngumu hapa duniani.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea:

www.salahallah.com
Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu…je, kinahusu moyo wako?
“Enzi yake imeenea mbingu; na ardhi; wala kuvilinda hivyo hakumshindi; na Yeye (peke yake) ndiye aliye juu na ndiye aliye Mkuu [kwenye utukufu].”
Al-Baqarah 255

Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu…

moyo wako!

Mfululizo no.26