Kiswahili 05. …‘Mwenyezi Mungu …asafishe yaliyo mioyoni mwenu.’

Assalamu’ alaikum

 

Kitu gani kimetokea ndani ya moyo wa mwanadamu? Mbona siku hizi kuna udanganyifu mwingi mno, rushwa, na uhalifu katika jamii? Hata wale wanaoonekana kana kwamba ni wanadini wema hawajaachwa wasipatwe na matatizo haya. Je, maradhi haya yametoka wapi? Hivi Mwenyezi Mungu aliiumba mioyo ya binadamu kuwa na ufisadi kama huo? Au ni wanadamu wenyewe waliochagua mambo kuwa hivyo? Haya ni baadhi tu ya maswali tunayotafuta majibu yake. Mwenyezi Mungu atatupa sisi majibu tunapovigeukia Vitabu Vitakatifu vilivyoteremshwa kwetu. Kabla kurasa takatifu hazijaanza kufunguliwa za hivyo Vitabu Vitakatifu, ni jambo la busara sana kuomba ushauri kutoka kwa yule Mmoja ambaye peke yake aweza kutupa sisi ufahamu sahihi. Sura 3:003

‘Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili. Zamani – ziwe uongozi kwa watu. Na akateremsha vitabu vingine vya kupambanua baina ya haki na batili.’ Al-Quran, 003:003 (Aali Imran).
Kurani Tukufu yatuambia sisi kwamba Sheria (Taurati) na Injili ni uongozi kwa watu. Mwenyezi Mungu ametupa nuru na uongozi katika kile ambacho Kurani Tukufu inakiita “Kitabu chake Mwenyezi Mungu” [yaani, Taurati ya Maandiko Matakatifu] Sura 5:44, hayo alipewa Musa. Walakini, Mungu hakukomea pale, pia alitupa sisi Injili kuwa uongozi, nuru, mauidha na kutuhakikishia yaliyoteremshwa kabla yake katika Taurati au Kitabu chake Mwenyezi Mungu. Kitabu cha Mwenyezi Mungu kinayo majibu tunayohitaji kwa maswali haya magumu. Kama Maneno yaliyoteremshwa kwetu katika Taurati na Injili yangekuwa hayajatoka kwa Mwenyezi Mungu, basi, Nabii Mstahiki Muhammad asingekuwa ametupa sisi mauidha mengi mno kutuelekeza sisi kwenye hivi Vitabu Vitakatifu. Kwa hiyo tunamwona Nabii Mstahiki Muhammad akituelekeza tena na tena kwenye Vitabu hivi Vitakatifu vya Maandiko ya Biblia. [Sura 5:44-48, Sura 21:48].
Jinsi Moyo wa Binadamu Ulivyopata Ugonjwa…
Wengi wenu mnakijua kisa cha Adamu, yule binadamu wa kwanza aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu. Kisa chote kimeandikwa katika Taurati (Mwanzo 1:26-31). Mwenyezi Mungu alikuwa amemuumba Adamu na mkewe wakiwa wakamilifu na watakatifu. Akawaweka katika bustani nzuri, bustani ambayo sisi hatujawahi kuiona kabisa. Hao wawili wakiwa watakatifu walipaswa kufurahia raha na utulivu wa mbinguni. Hakuna cho chote kilichovuruga amani yao. Asili zao zilikuwa safi, mawazo yao yalikuwa matakatifu. Mwenyezi Mungu aliwapa vitu vyote walivyoweza kuhitaji katika bustani hii nzuri ili kuwafurahisha. Waliruhusiwa kula matunda ya miti yote waliyopewa kuwa chakula chao … isipokuwa ule mmoja. Kitu kimoja tu walizuiwa … yaani, walikatazwa wasile matunda ya ‘mti wa ujuzi wa mema na mabaya’ uliokuwa katikati ya bustani ile. Taurati (Mwanzo 2:15-17) ‘Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.’ Hili lilikuwa ni jaribio tu la imani kuona kama mtu yule ataweza kutegemewa.
Mambo yote yakawaendea vizuri, mume yule na mkewe, ambao walikuwa watakatifu katika bustani ile ya raha (peponi) isipokuwa siku ile walipoasi. Amri ya Mwenyezi Mungu ya kutokula mti ule uliokatazwa ikakiukwa, wakati walipoanguka katika majaribu ya yule nyoka. Sasa mawazo yake Adamu hayakuwa safi tena kwa asili yake kama yalivyokuwa hapo mwanzo, bali yakawa maovu. Tangu siku ile hadi siku hizi zetu dhambi imewaletea wanadamu wote laana. Kwa kuwa sisi tu watoto tuliotoka kwa Adamu, sisi pia tumerithi asili yake iliyoanguka dhambini. Katika Taurati tunaambiwa juu ya hali yetu ilivyo hasa. Yeremia 17:9 ‘Moyo [wa mwanadamu] huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?’
Uponyaji unavyokuja…
Mioyo yetu (mawazo yetu) haiwezi kutegemewa, hatuwezi kuangalia ndani yetu wenyewe na kudhani twaweza kutatua matatizo yetu. Hakuna tiba ya kibinadamu iliyopatikana kutibu hali ya dhambi iliyo ndani ya moyo wa mwanadamu. Lakini, je! hivi mwanadamu huyu ameachwa pasipo tumaini? Mwenyezi Mungu kwa rehema zake na huruma zake hakumwacha mwanadamu katika hali isiyo na matumaini. Mwenyezi Mungu ameahidi kutusaidia. Je, haya yafuatayo si maneno ya faraja,… “Mwenyezi Mungu ili ayadhihirishe yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyo mioyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua (hata) yaliyomo vifuani.” Al-Qur’an, 003:154 (Aali Imran). Ni Mwenyezi Mungu anayechukua hatua ya kwanza kumsaidia mwanadamu. Hata hivyo, mwanadamu sharti atake kusafishwa, yaani, apate utakaso utokao kwa Mwenyezi Mungu. Mwanadamu hana budi kuomba kwa ajili ya jambo hilo, na kulitafuta kwa uwezo wake wote. Lakini je, huko kutakaswa kwa moyo wa kibinadamu kunawezaje kufanyika na kwa njia ya nani? Kurani Tukufu inaongea juu ya Mmoja aliyeteremshwa hapa chini kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mmoja wa pekee aliyekuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu, jina lake ni Isa al- Masih. “(Kumbukeni) waliposema Malaika: “Ewe Maryamu! Mwenyezi Mungu anakupa habari njema (za kumzaa mtoto bila ya mume, bali kwa kutamkwa) Neno tu litokalo kwake (la kukwambia ‘Zaa’ ukazaa pasina kuingiliwa). Jina lake ni Masihi, Isa, mwana wa Maryamu, mwenye heshima katika dunia na Ahera, na miongoni mwa waliopelekwa mbele na Mwenyezi Mungu.” 003:045 (Aali Imran).
Twasoma kwamba Isa al-Masih alikwenda huku na huku akiwa na huruma kwa watu, akiponya magonjwa yao. Je, yawezekana kwamba huyu Mmoja aliyeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu angeweza pia kuponya ugonjwa wa moyo? Twasoma katika Injili, kwamba wote waliokuja kwake Isa al-Masih kwa uponyaji wa matatizo ya kimwili na kiakili walipewa msaada. Hakuna hata mmoja aliyefukuzwa. Twasoma katika Vitabu Vitakatifu, (Injili) Marko 1:41 “Naye [Isa al-Masih] akamhurumia [mwenye ukoma], akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.” Je, hivi kungekuwa na uwezekano pia kwamba Mwenyezi Mungu afanye ipatikane tiba ya ugonjwa uliomo ndani ya moyo wa mwanadamu kwa ajili yetu kupitia kwa mtu yuyo huyo Isa al-Masih? Katika Injili tunaambiwa tena, 1 Yohana 1:7 ‘Bali tukienenda nuruni, kama yeye (Isa al-Masih) alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu (Isa al-Masih), Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”
Hili ni jambo tunaloweza kulionja sasa hivi. Kusafishwa mazoea yote mabaya na matendo mabaya, hata na mawazo yetu machafu yanayotushikilia katika maovu. Mazoea yetu mabaya yawe ni mawazo maovu au matendo maovu, kusema uongo, kukosa uaminifu, uzinzi, yote haya, na mengine mengi, Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo mioyoni mwetu. Mwenyezi Mungu analo suhulisho, tena ameahidi kutuweka huru mbali na maradhi hayo ya dhambi. Hii ndiyo maana Isa al-Masih anaitwa “Masihi” “Mwokozi” atuokoaye sisi kutoka katika dhambi. Siyo tu kwamba Isa alilipa fidia kwa ajili ya dhambi zetu, bali pia mtu huyu aliyeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu alituahidi kutupa sisi moyo mpya, kuponya ugonjwa katika mioyo yetu iliyoanguka dhambini. Twapokea msaada tu tukienda kwake Mwenyezi Mungu na kwake Yeye ambaye Mwenyezi Mungu alimteremsha chini. Tena kutoka katika Injili … 1 Tim. 2:5-6 twasoma: “Kwa sababu Mungu ni Mmoja, na mpatanishi (Shafi) kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu (Isa al-Masih); ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote”..,
Usafishaji huo wa moyo ni mkamilifu jinsi gani?
Kwa kiwango kile cha kuyageuza hata mawazo yetu yenyewe! 2 Wakorintho 10:5 [Injili] ‘Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu (Allah); na kukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo [Isa al-Masih]…’
Tena katika Injili, imeandikwa katika Matendo 3:26 “Mungu (Allah), akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu [Isa al-Masih], alimtuma kwenu ninyi kwanza [Waisraeli], ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu [dhambi] yake.”
Huko nyuma katika siku zile mbali watu hawakumtaka Mwokozi kama huyo, walichagua kubaki katika dhambi na kubaki na ugonjwa wa moyo ambao ulianguka dhambini. Kwa kweli wale walioutangaza ujumbe huu wa uhuru walichukiwa na Wayahudi, sana sana kiasi kwamba wengi walifungwa gerezani na hata kuuawa. Hiyo ilikuwa ndiyo chuki dhidi ya wale waliompokea Yeye ambaye Mwenyezi Mungu alimteremsha kuja katika dunia hii. Kwa kweli wafuasi wake Isa al-Masih walinena kwa ujasiri mno kiasi cha kutangaza kwamba… “wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Matendo 4:12 Injili. Basi, kwa heshima yake, je, waona ni ajabu kwamba Muhammad aliitaja Injili … yaani, kwamba hii ilikuwa ndiyo ‘injili’ au habari njema iliyoteremshwa chini kutoka kwake Mwenyezi Mungu kupitia kwa Isa al-Masih? Kwa nini Nabii Mstahiki Muhammad amtaje Isa al-Masih katika Sura zipatazo kumi na tano pamoja na kumtaja Isa zaidi ya mara 90 katika Kurani Tukufu? Hakika habari zilizo katika Injili ni “Habari Njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu”. Sura 3:45
Moyo wako uwezavyo kupokea mbaraka huo…
Moyo wa zamani wenye dhambi hauna tiba ya kibinadamu… Tujaribu sana kama tuwezavyo kwa kutenda matendo mema, na kuwapa maskini msaada, na kuomba mara kwa mara na kwa muda mrefu … hata hivyo mambo hayo hayawezi kuyatakasa maisha yetu.
Hatuwezi kuugeuza moyo wetu wa kibinadamu kwa kutenda matendo mema na kuomba sala ndefu … Mwenyezi Mungu peke yake ameahidi kuuponya moyo huo mgonjwa kwa kutupa sisi moyo mpya … (Taurat) Ezekieli 36:26 ‘Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami [Mwenyezi Mungu] nitatoa moyo wa jiwe [mgumu na uliojaa ufisadi] uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.’
Hivi twawezaje kuwa na huo ‘moyo mpya’? Kwa kumwomba tu Mwenyezi Mungu! Nenda kwake faraghani na kufanya maombi (dua) au wakati unapokuwa Msikitini. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa rehema, mpole, na mwenye huruma kwa watoto wote wa wanadamu. Lakini hatumii nguvu kuja kwetu. Katika Kurani Tukufu amesema … ‘Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika dini. Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa shetani na akamwamini Mwenyezi Mungu, bila shaka yeye ameshika kishiko chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.’ Sura 2:256 (Al Baqarah).
Vivyo hivyo Mungu hatatumia nguvu juu yetu, anapaswa kuombwa. Mjumbe wake wa kibinadamu peke yake sharti afanye uamuzi na kumwomba. Mwanadamu sharti achague nani atakayekuwa Bwana wake. Ama ni Mwenyezi Mungu kupitia kwa Isa al-Masih, ama, ni Shetani (Ibilisi) yule aliyeanguka, ambaye ni laghai mkuu. Mamlaka zote za Mbinguni zinahusika katika kukusaidia wewe kufanya uamuzi huo. Mwombe leo hii! Shika ‘kishiko kile chenye nguvu kisichokuwa na kuvunjika’.

Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913.

Mafungu ya Biblia yametolewa kutoka katika Toleo la King James (KJV)

www.salahallah.com

‘Mwenyezi Mungu … asafishe yaliyo mioyoni mwenu.’

Sura 3:154
Aali Imran

Mfululizo na. 05