Kiswahili 06. Siku Litakapopulizwa Parapanda!

Assalamu’ alaikum

 

Wengi siku hizi katika dini ya Kiislamu husadiki kwamba Isa al-Masih [Kristo Masihi] atarudi. Lakini Isa al-Masih anaporudi, tutajuaje sisi kwamba ni Yeye mwenyewe kweli? Twawezaje kujua kama huyo si tapeli?
Matapeli wa Ibilisi…
Kumbukeni kwamba Ibilisi (Shetani) amejaribu kuigiza kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu ametenda. Hebu kwa mfano tu, katika Taurati, Mwanzo 1:1 tunaambiwa kwamba “Hapo mwanzo Mungu (Allah) aliziumba mbingu na nchi.” Kurani Tukufu yatuambia sisi hivi:
Sura 32:4

“Mwenyezi Mungu ndiye Aliyeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, katika nyakati sita (anazozijua Mwenyewe Mwenyezi Mungu); na Akatawala katika Arshi yake. Ninyi hamna mlinzi wala muombezi isipokuwa yeye tu, je hamfikiri?” 032:004 As-Sajdah
Walakini sisi tunaona kwamba wengi hata miongoni mwa waumini wanasema kwamba hivyo sivyo mambo yalivyo, wanasema kwamba dunia, mwanadamu na wanyama ‘wameibuka’ tu katika kipindi cha mamilioni ya miaka kilichopita. Imani isemayo kwamba Mwenyezi Mungu aliviumba vitu vyote katika maumbile yanayotuzunguka haingii katika mawazo ya wengi. Hivyo Neno lake Mwenyezi Mungu huwekwa kando ili kuzifuata hadithi hizi za uongo zilizotungwa na wanadamu. Lakini hizi hadithi za uongo ambazo ni kinyume cha kweli na hupokewa badala ya ile kweli ya Mwenyezi Mungu. Hivyo nadharia ya kuibuka kwa vitu (evolution) ni ya uongo na inawapoteza watu wengi. Hii ni kazi yake Ibilisi (Shetani).
Katika Taurati, Mwanzo 1:26 imeandikwa kwamba Mwenyezi Mungu alisema … “Na tufanye mtu kwa mfano wetu…” Lakini leo watu wanalishwa ukweli wa uongo, watu wengi wenye akili nyingi leo wanasema kwamba sisi tulitoka kwa nyani zamani sana … jambo ambalo tena ni uongo wake Ibilisi [Shetani]. Ni dhahiri kabisa kwamba Ibilisi [Shetani] analichukia Neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, Vitabu Vitakatifu, na waliotumwa na Mwenyezi Mungu. Tunaweza kuhakikishiwa ya kwamba Ibilisi (Shetani) atajaribu pia kuigiza Kuja Mara ya Pili kwa Isa al-Masih! Kwa njia hii ataweza kuwadanganya watu wengi na kuwapotosha kutoka katika ile njia nyofu ya Mwenyezi Mungu. Kama vile tu ambavyo tayari yeye amekwisha kuwadanganya wengi kwa nadharia ya “Uibukaji wa Vitu” na dhana yake isemayo kwamba wanadamu walitoka kwa “nyani”, ndivyo atakavyowadanganya wote wanaogeukia kando na kuviacha Vitabu Vitakatifu vilivyoteremshwa kwetu. Lakini Mwenyezi Mungu katika wema wake, huruma zake, na rehema zake kuu tayari ameteremsha kweli yake kabla ya wakati ili tujue hila au madanganyo ya Ibilisi [Shetani]. (Injili) Mathayo 24:4 “Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye.” Mara tano katika Injili tunaonywa tusidanganywe!
Kweli Zake Mwenyezi Mungu…
Vitabu Vitakatifu, Maandiko ya Biblia, yana mengi ya kusema kuhusu Marejeo yake Isa al-Masih. Watu wake Mwenyezi Mungu watakuwa wanatazamia kurudi kwake Isa al-Masih (Kristo Masihi). Haya yametabiriwa katika: (Injili) Waebrania 9:28 ‘kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, … kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.’
Lakini kabla Isa al-Masih hajarudi twaweza kuwa na hakika kwamba Shetani (Ibilisi) atajaribu kuigiza kuja Kwake, hata mamilioni watadhani kwamba (Shetani) ndiye Isa al-Masih [Kristo Masihi] mwenyewe. Safari moja mimi nilipewa noti ya bandia na dereva wa taksi, na katika pilikapilika za siku ile, sikuiangalia kwa karibu noti ile mpaka baadaye jioni ile nilipostarehe katika chumba changu hotelini. Nilipokuwa nikiangalia fedha zangu niliona kitu fulani kilichokuwa tofauti kuhusu noti hii moja niliyokuwa nimeipokea. Nilipoichunguza niliona kwamba kweli noti ile ilikuwa ya bandia. Nilikuwa nimedanganywa! Hata hivyo nilijinusuru na hali ile kwa vile ilikuwa ni noti ndogo na haikuwa ya maana sana katika maisha yangu. Lakini, kuhusu tukio hili kuu la kuja Mara ya Pili kwa Isa al-Masih, hatuthubutu kudanganywa. Tumeonywa vya kutosha katika Injili kwamba Makristo wa uongo watatokea na kuwadanganya wengi. Mwenyezi Mungu katika rehema zake tayari ameteremsha maonyo kabla ya wakati ule, ili pasiwepo na haja ya sisi kudanganywa.
(Injili) Mathayo 24:5 “Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi.” (Injili) 2 Wakorintho 11:13-14 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu,. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.” Kristo huyu wa uongo atakuja kuudanganya hata ulimwengu wote. Zingatia maneno yaliyo katika (Injili) Mathayo 24:30 “ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.” Kumbuka kwamba “mataifa yote ya ulimwengu [ndipo] watakapoomboleza”. Kwa nini waomboleze? Je, ni kwa sababu walimkubali kristo yule wa uongo, yule tapeli, na sasa yule wa kweli anaonekana mawinguni akiwa na nguvu na utukufu mwingi, wanatambua walifanya kosa kubwa mno? Lakini ole wao wamechelewa sana! Rafiki zangu, bado hatujachelewa sana twaweza kuijua kweli! Tafadhali endelea kusoma.
Je, Isa al-Masih Atarudije?
Katika Ufunuo wake Isa al-Masih aliouteremsha kwa Yahaya [Yohana kisiwani Patmo] tunaona yameandikwa haya kuhusu kurudi kwa hakika kwa Isa al-Masih [Kristo Masihi].
(Injili) Ufunuo 1:7 “Tazama, [Isa al-Masih] yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake…” Inatuhakikishia sisi bila shaka lo lote kwamba “kila jicho litamwona” na kuja kwake ni pamoja na “Mawingu”. Tena inatuambia kwamba ‘kabila zote za dunia wataomboleza’ kwa kuwa walidanganywa na tapeli. Isa al-Masih pia anakuja kama “Umeme”. Imeandikwa katika Injili … Mathayo 24:27 “Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” Kuja kwa Isa Mara ya Pili kutaonekana kwa watu wote ulimwenguni. Hakutakuwa kwa siri mahali fulani pasipojulikana, bali kutakuwa kwa wazi. Hutahitaji kwenda kwenye televisheni au kwenye Interneti kuliona tukio hilo. Utaliona ukiwa nje ya mlango wa nyumba yako!
Jambo jingine la kushangaza kuhusu tukio hili ni kwamba kutakuwako na ufufuo kutoka makaburini. (Injili) 1 Wathesalonike 4:16 hutuambia kwamba … “Kwa sababu Bwana [Isa al-Masih] mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.’ Tukio hili halitaonwa tu na kila jicho, bali litasikiwa na kila sikio. Zingatia kwamba kuja huku kwa Isa al-Masih ni kwa “mwaliko” na “sauti ya malaika mkuu” na “parapanda” au tarumbeta ya Mungu. Kile kinachojidhihirisha katika fungu hili ni kwamba “waliokufa katika Kristo” watafufuliwa kwanza. Huu ndio ufufuo wa waumini wa kweli kutoka makaburini mwao. Kufufuliwa? Kufufuliwa waende wapi? Kule juu mawinguni kuwa pamoja na Isa al-Masih milele zote.
(Injili) 1 Wathesalonike 4:17 “Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao [wale waliofufuliwa kutoka makaburini mwao] katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Huu ni usemi mzito … “kumlaki Bwana hewani”. Tusipoteze jambo hilo, Isa al-Masih haji mara yake ya pili kusimama juu ya dunia hii kama alivyokuja zamani, Aja kuwakusanya waumini waende kwake mwenyewe “hewani”. Hii ni kazi ya kuokoa maisha itokayo nje ya sayari hii iliyochafuliwa kutokana na mambo ya uongo na madanganyo ya Ibilisi [Shetani].

Dalili za Kuja Kwake Isa…
Twawezaje kuwa na hakika kwamba kuja kwake kumekaribia? Je, kutakuwa na dalili zo zote kwa ajili yetu tupate kujua kwamba kuja kwake kumekaribia? Dalili moja aliyotuambia Isa al-Masih ni kwamba itakuwa kama zilivyokuwa siku za Nuhu kabla ya gharika na kama siku zake Lutu… (Injili) Luka 17:26-30 “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu [Isa al-Masih].”
Ni kwa jinsi gani tu hali ilikuwa mbaya katika siku zile kabla ya gharika? (Taurati) Mwanzo 6:5 “BWANA (Allah) akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.”
Maovu yakiwa yamekithiri, kila wazo la moyoni (akilini) likawa ovu tu sikuzote. Je, hali hiyo haielezei siku zetu zilivyo pia? Kwa hiyo twaweza kutegemea kuja kwake upesi sana Isa al-Masih, kuja kukomesha maovu haya ya kutisha, yaani, wenda wazimu huu,

Sura 27:087

‘Na (wakumbushe) siku litakapopulizwa parapanda, (baragumu) la Kiama); wahangaike waliomo mbinguni na waliomo ardhini ila yule ambaye Mwenyezi Mungu (anataka asihangaike), (asifadhaike); na wote watamfikia (Mwenyezi Mungu), hali ya kuwa wadhalilifu.’ 027:087 An-Naml
Je, hivi wewe na mimi tutakuwa tayari kwa ajili ya siku ile? Mkabidhi maisha yako Yeye aliyeteremshwa na Mwenyezi Mungu kuja hapa chini, yaani, Isa al-Masih, awe Mwokozi wako akuokoaye kutoka dhambini.

Aya hizi zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913

Maandiko ya Biblia yanatoka katika Toleo la King James (KJV)

Kwa habari zaidi:

www.salahallah.com

‘Siku
Litakapo-pulizwa
Parapanda!

Sura 27:87
An-Naml

Mfululizo na. 06