Kiswahili 03. ‘Habari Njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu’!

Assalamu’ alaikum

 

Kwa kweli hata Neno moja tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu lingekuwa Habari Njema! Watu wangepaswa kushukuru jinsi gani kupokea kitu cho chote kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Yeye ni mwingi wa rehema na Mpole anaposhughulika na wanadamu. Tunaambiwa katika Kurani Tukufu kwamba Yeye mwenyewe alituteremshia sisi huyo ‘Neno’ na jina lake alikuwa ni Kristo Yesu. (Isa al-Masih).
Sura 3:45

‘(Kumbukeni) waliposema Malaika: “Ewe Maryamu! Mwenyezi Mungu anakupa habari njema za (kumzaa mtoto bila ya mume, bali kwa kutamkwa) Neno tu litokalo kwake la kukwambia ‘Zaa’ ukazaa pasina kuingiliwa). Jina lake ni Masihi, Isa, mwana wa Maryamu, mwenye heshima katika dunia na Ahera, na miongoni mwa waliopelekwa mbele na Mwenyezi Mungu.”
Kwa hakika hizi ni “Habari Njema” kweli kweli. Ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye mkuu, Muumbaji wa malimwengu aweze hata kuinama chini kuwasiliana na mwanadamu aliyeanguka (dhambini) ni maajabu tuyatazamapo! Hilo lingeweza tu kuwa pendo lake kuu mno na huruma zake zisizo na kikomo alizo nazo kwa kila mmoja wetu binafsi!
Mwenyezi Mungu anahangaika sana kwa ajili yetu, kiasi kwamba kwa Rehema zake alichagua kumteremsha mmoja anayeheshimiwa na aliye karibu sana naye. Sura 3:45. Kwa hakika kabisa Kurani Tukufu haiwezi kukosea.

Katika Sura 5:46 twaambiwa kwamba Yesu (Isa al-Masih) aliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuihakikisha Sheria na Injili (Taurati na Injili), ambamo ndani yake umo Uongozi na Nuru. Siyo tu inatuambia sisi kwamba Taurati na Injili vilihakikishwa, bali pia inatuambia katika Sura 5:48 kwamba hayo Maandiko (Biblia ) yali“lindwa”. Hivyo Muhammad (jina lake na liheshimiwe), alikuwa akiwaelekeza kwenye Neno lililotoka kwa Mwenyezi Mungu wale walioitafuta kweli. Kwenye Uongozi huo na Nuru hiyo tunamwelekeza msomaji, yaani, kwenye Injili ambayo katika Waebrania 1:3 inasema kwamba Isa al-Masih (Kristo Masihi) “ni … chapa ya nafsi Yake [Mwenyezi Mungu], akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, … aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu.”
Karibu sana na Mungu Mwenyezi!
Ni kweli iliyoje kwamba Isa al-Masih (Kristo Masihi) baada ya kuwa hapa duniani, aliketi mkono wa kuume wa Mungu [Allah], na yuko ‘karibu sana na Mwenyezi Mungu’. Sura 3:45
Kwa vile sisi tumeanguka, yaani, tu wenye dhambi, tu viumbe na katika hali yetu ya dhambi hatuwezi kumwona Mwenyezi Mungu na kuwa hai, bado tunahitaji kuwa na ufahamu ili tujue alivyo Mwenyezi Mungu. Katika Injili, Yohana 1:18, tunaambiwa kwamba ‘Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote’ … ni Kristo (Isa al-Masih) pekee inasema … ‘aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.’ Wanadamu hawawezi kumtazama Mwenyezi Mungu na kuwa hai, hata hivyo Mwenyezi Mungu kwa Rehema zake alimteremsha Mmoja aliyekuwa “katika kifua” chake Mwenyewe na ambaye yuko karibu sana naye, kuwa “chapa” ya jinsi Mwenyezi Mungu alivyo hasa.
Tuna upendeleo ulioje kuweza kuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyo hasa. Katika maisha ya Isa al-Masih tunao Upole na Huruma za Pendo lake Mwenyezi Mungu linalodhihirishwa kwa ukamilifu kabisa kwa wanadamu. Maneno yake Isa mwenyewe katika Injili yalikuwa ni haya … “Aliyeniona mimi amemwona Baba” (Yohana 14:9). Sasa twaweza kuwa na picha bora zaidi kuhusu alivyo Mwenyezi Mungu, ikiwa imejengwa juu ya maisha yake Isa al-Masih.
Je! hivi kuna ajabu yo yote kwamba Kurani Tukufu Sana ndani yake yenyewe inazo zaidi ya aya 90 zisemazo wazi kabisa juu ya Isa (Kristo Masihi). Sura kumi na tano katika Kurani Tukufu hunena habari zake Yeye. Nabii Muhammad alijua fika umuhimu wa kumwelewa Isa al-Masih kuwa ni nani, vinginevyo asingekuwa amenena habari zake katika Sura nyingi sana za Kurani Tukufu. Sisi tungefikiriwa kuwa tumebarikiwa sana endapo tungetumia muda wetu kumfahamu Mtu huyu mashuhuri sana kama kumbukumbu zake zilivyoandikwa katika Injili.
Katika Injili ya Maandiko ya Biblia, twasoma jinsi Isa al-Masih alivyokwenda huku na huku akiponya magonjwa na maradhi ya kila namna, wanaume, wanawake, watoto hata na wale wenye ukoma waliponywa na kuwa wazima. Mara nyingi walemavu waliponywa na wafu wakawa hai. Ni furaha iliyoje hiyo iliyoletwa na mambo hayo miongoni mwa watu! Isa al-Masih alipotembea katika njia zenye vumbi toka kijiji kimoja hadi kijiji kingine, huruma yake kwa mwanadamu aliyeanguka (dhambini) ilijidhihirisha waziwazi.. Alikuja kumfunua alivyo hasa Mwenyezi Mungu. Ndani yake Isa al-Masih (Kristo Masihi) twaona picha yake Mwenyezi Mungu ambayo kabla yake ilikuwa haijapata kufunuliwa kamwe kwa kina kama hicho.
Kurani Tukufu yaendelea kutuambia sisi kwamba wale wamfuatao Kristo (Isa al-Masih), Mwenyezi Mungu a‘tawaweka wale waliokufuata, juu ya wale waliokufuru.’ Sura 3:55. Rafiki zangu, je, si jambo la maana, basi, kufanya uchunguzi juu ya maisha ya Mtu huyu aliyeteremshwa na Mwenyezi Mungu? Ikiwa Nabii Muhammad (jina lake na liheshimiwe) alisema juu ya wale wamfuatao Isa al-Masih kuwa wangewekwa juu ya wale wanaokufuru, basi, ni halali kabisa kwetu kujua habari zake huyo Isa (Kristo Yesu) na pia kuwa wafuasi wake.
Kwa kutuhakikishia, Kurani Tukufu inatuambia sisi kwamba wale walio wanafunzi wa (yaani, wamfuatao) Isa (Kristo Masihi), yaani wasaidizi hao wa Mwenyezi Mungu, wangepaswa kuitwa ‘wamejisalimisha’ kwake. Sura 3:52
Sisi sote twajua kwamba “Mwislamu’ ni mtu mmoja ambaye amejisalimisha na kumtii Mwenyezi Mungu. Utii huu hauna swali wala haubakizi kitu kwa upande wetu. Utii huu ni lazima utolewe pia kwa Neno (Isa al-Masih) aliyeteremshwa kuja kwetu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbuka Sura 3:45 isemayo kwamba Mwenyezi Mungu “anakupa … Neno tu litokalo kwake … Jina lake ni Masih, Isa,” Kwa maana Mwenyezi Mungu, Aliye Mtakatifu, asingefanya mambo yote hayo yaliyo ya lazima kumteremsha Neno wake kuja kwetu katika maisha ya Isa al-Masih kama jambo hilo lisingekuwa la maana.
Hebu tu na tuwaze hivi, endapo wewe ungepata heshima nyingi sana kutoka kwa mfalme wa nchi, naye amtume kwako mwakilishi wake, yaani, mmoja ambaye yu karibu sana na huyo mfalme. Mwakilishi wake huyo anapowasili na kutaka kusema nawe, kungetokea nini kama ungemdharau mtu huyo? Je! hilo lisingekuwa tusi la kutisha kwa mfalme? Hebu sikiliza, ewe rafiki yake Mwenyezi Mungu, kwa njia iyo hiyo, Mungu wa Mbingu na Dunia ametuteremshia Neno wake kweli kweli kuja kwetu, katika umbile la Isa al-Masih (Kristo Yesu). Asingekuwa mtu ye yote tu bali ni yule Neno (Isa al-Masih) ambaye yu karibu na Mwenyezi Mungu kuliko wote, naye anatoka katika “kifua” cha Baba. Mtu huyo wa maana sana, atokaye katika kifua cha Mwenyezi Mungu, hatuna budi kumjali kwa njia ya pekee, vinginevyo, sisi nasi tutaonekana kuwa tunamtolea matusi makubwa sana Mwenyezi Mungu.
Isa al-Masih alipokuwa kando ya mto Yordani ili kubatizwa na kuwa kielelezo kwetu, Maandiko yanatuambia sisi kwamba mbingu zikamfunukia na sauti yake Mungu ikasikika … (Injili) Mathayo 17:5 ‘Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.’ Maneno hayo mawili ya mwisho, ‘msikieni yeye’ ni ya muhimu kwetu kwamba tusikilize yale ambayo Mwenyezi Mungu ametuteremshia ndani ya Isa al-Masih!
Injili, ambayo Muhammad alituambia kwamba iliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Sura 3:3, ina mafungu ya maneno ya Maandiko ambayo yanarudia kusema baadhi ya mawazo yale yale yapatikanayo katika Sura 3:45 ambayo hunena juu ya Isa al-Masih kuwa ndiye ‘Neno aliyeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu’. Angalia kile isemacho katika Yohana 1:1 ‘Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu [Allah], naye Neno alikuwa Mungu [Allah].’ Kisha inaendelea kutuambia sisi kwamba “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa [akateremshwa] kwetu” fungu la 14. Ni huyu Neno aliyetuonesha sisi jinsi Mwenyezi Mungu alivyo hasa.
Huyu si mwana aliyezaliwa kimwili kama watu leo walivyo na watoto. Lakini huyu ni yule Mmoja aliyezaliwa na bikira, ambaye alikuwa bado hajamjua mume. Kumbuka kwamba hakuna neno lo lote lililo gumu kwa Mwenyezi Mungu! Yeye aweza kusema tu na mambo yakawa vile. Soma tena Sura 3:46
Je! huyo ni Mwanawe Mungu (Allah)?
Huenda umewahi kusikia usemi huu “mwana wa njia”, je, njia ina mwana? La, hasha, lakini maana yake hapa ni kwamba mtu yule anayekidhi maelezo hayo ni msafiri. Usikate tamaa unaposikia kifungu hiki cha maneno “Kristo, Mwana wa Mungu” hii haimanishi kwamba Mungu [Allah] anaye mwana aliyemzaa kwa njia ile ile wanadamu wanavyozaa watoto, kwa maana hilo kamwe haliwezi kuwa hivyo. Lakini kinamtaja Kristo kuwa ni Mwana kwa maana ile ambayo Isa yuko karibu sana na Mwenyezi Mungu na ni kwa njia ya Isa (Kristo) tabia ya Mwenyezi Mungu inadhihirishwa kwetu vizuri sana. Njia iliyo wazi kabisa na bora kabisa kwa Mwenyezi Mungu kuwasiliana na wanadamu ni kumtumia mmoja anayefanana na sisi! Hivyo Yeye ndiye Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu …”msikieni yeye”.

Kichaka Kilichowaka Moto
Mpendwa rafiki usifikiri hata kwa dakika moja kwamba Mwenyezi Mungu amewekewa mipaka na hawezi kufanya hili. Kumbuka kisa cha Musa na kichaka kilichowaka moto. Kinatuambia kwamba Mwenyezi Mungu alinena na Musa kutoka katika ule moto. Kama Mwenyezi Mungu anaweza kuja kwa mfano wa kichaka kinachowaka moto, je! hawezi pia kuja katika umbile la Mwanadamu na kujidhihirisha Mwenyewe kwetu na kunena nasi? Ni hakika kabisa hakuna kitu cho chote kilicho kigumu kwa Mwenyezi Mungu!
Mwenyezi Mungu na akubariki sana unapotafuta kufanya mapenzi yake na kuchagua kutii kile alichokudhihirishia wewe. Ni kweli Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndani ya Kristo Masihi hizo kwetu ni “Habari Njema” ‘msikieni yeye’! Bismillahir rahmanir rahim”.
Kabla hujafungua kurasa za Vitabu Vitakatifu, daima omba Mwenyezi Mungu akufundishe kuwa na ufahamu sahihi usomapo. Mwenyezi Mungu anawabariki wale wanaojifunza kwa unyofu wa moyo na wanaoitafuta haki. Yeremia 29:13 ‘Nanyi mtanitafuta, na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.’ Wale wamtafutao Mwenyezi Mungu, hawana budi kumtafuta kwa moyo wao wote.
Al-Baqara 002.153
‘Enyi mlioamini! Jisaidieni (katika mambo yenu) kwa subira na Sala; bila ya shaka Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.’

Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913

Mafungu ya Biblia kutoka Toleo la King James (KJV)

Kwa maelezo zaidi au mauidha tafadhali wasiliana na:
www.salahallah.com

‘Habari Njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu’

Sura 3:45
Aali Imran

Mfululizo na. 03