Kiswahili 09. ‘Acheni Dhambi Zilizo Dhahiri na Zilizofichikana’ …

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

 

Amani ya Mwenyezi Mungu na iwe juu yenu na tena apate kuyaongoza maisha yenu. Somo letu leo linahusu Sheria ya Mwenyezi Mungu , – “Sharia ya Allah” – (Amri Kumi). Siku hizi watu husema kwamba Mwenyezi Mungu hana Sheria yo yote! Hata kutoka miongoni mwa waumini wamo wengi wasemao kwamba Sheria ya Mwenyezi Mungu, (kama ilivyoandikwa katika zile Amri Kumi) haiwafungi tena wanadamu leo. Je, ni kweli wanadamu wanaweza kuishi pasipo sheria zo zote?
Taifa Lisilokuwa na Sheria…
Hebu na tuseme taifa fulani linachagua kufutilia mbali sheria zote. Kila mtu yu huru kuchagua kile akitakacho. Je, tungeweza kuona picha ya taifa, kwa mfano, lisilokuwa na sheria za usalama barabarani? Au hata vibaya zaidi, liwaondoe maofisa wote wa polisi wasifanye kazi zao za kusimamia sheria? Je, jambo hilo lisingeleta machafuko mabaya mno? Hakuna cho chote ambacho kingekuwa salama, maisha yangegeuka na kuwa matukio ya kuogofya sana. Wezi wangetwaa kile kilicho mali ya mwingine bila kujali maisha yake. Hakika maisha kama hayo yasingeingia mawazoni. Lakini, kwa sababu fulani watu wanajisikia kwamba ile Sheria ya Mwenyezi Mungu ya Amri Kumi haiwafungi wanadamu tena! Hebu fikiria mtu akisema, ‘Mwenyezi Mungu hajali mimi ninapokuwa na miungu mingine’, au ‘ni sawa tu kuiba’, au kwamba ni sawa kusema uongo kwa jirani yako au hata vibaya zaidi kupora mke wake au mali zake alizo nazo. Jumuia kama hiyo kwa hakika ingetoweka upesi.
Rafiki zangu, je, imepata kuwazukia wanadamu kwamba sababu ya ulimwengu huu kuwa na hali ngumu kama hii ni kwa kuwa watu wengi mno wameiweka kando Sheria ya Mwenyezi Mungu ya Amri Kumi (Sharia ya Allah) kama inavyopatikana katika Taurati, Kutoka 20. Katika Sura 2:93 twakumbushwa juu ya Sheria ile iliyotolewa.

002:093 ‘Na (kumbukeni habari hii kadhalika) Tulipochukua ahadi yenu (wazee wenu) na tukauinua mlima juu yenu (tukakwambieni): “Kamateni kwa nguvu haya tuliyokupeni na sikilizeni (hiyo Sheria)…” Sura 002:093 Al Baqarah
Je, Nabii huyu Mstahiki angeweza kuwaambia wasomaji wake ‘kamateni kwa nguvu haya tuliyokupeni na sikilizeni (hiyo Sheria)’, yaani, (Amri Kumi), kama yeye mwenyewe alikuwa haikubali ile Sheria kwa moyo wote? Je, isingefikiriwa kuwa ni kufuru kusema ‘kamateni kwa nguvu ile Sheria’, na huku yeye mwenyewe angekuwa anaihalifu Sheria Takatifu ya Mwenyezi Mungu katika maisha yake? Je, huu si wakati wa kuwa wakweli sisi wenyewe na kukubali kwamba vema, hapa ndivyo isemavyo kuhusiana na Sheria ya Mwenyezi Mungu! Katika Kurani Tukufu, twaambiwa kuacha dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana.

006:120 ‘Na acheni dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana. Hakika wale wanaochuma dhambi watalipwa yale waliyokuwa “wakiyachuma”’. Sura 006:120 Al An-am
Hapo zamani, watu wale wa kale kutoka Mashariki, walitambua fika maana ya ‘kuacha chambi.’ Watu hao wacha-Mungu walitambulikana katika Taurati, (Vitabu Vitakatifu) Ayubu 1:1 hunena habari za mtu mmoja aliyeitwa ‘Ayubu’. “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu,[Allah] na kuepukana na uovu.” Ayubu 1:1 (Maandiko ya Biblia). Anatambuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa “mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki’ Ayubu 1:3. Angewezaje mtu huyu kujua dhambi ni kitu gani, kama asingekuwa amefundishwa? Angewezaje kujua dhambi ni nini isipokuwa kama alikuwa ameijua Sheria ya Mwenyezi Mungu? Sisi twawezaje kujua dhambi ni nini isipokuwa kama tunaiangalia Sheria yake Mwenyezi Mungu? Dhambi yawezaje kufafanuliwa? Kwa hiyo Sheria [Amri Kumi] inahitajika ili sisi tupate kufahamu maana ya dhambi. (Injili) 1 Yohana 3:4 (TEV) “Kila mtu atendaye dhambi anavunja Sheria ya Mungu (Allah), maana dhambi ni uvunjaji wa Sheria.”
Sheria hii imewekwa kwa ajili ya furaha ya mwanadamu. Kama watu mahali pote wangeitii, wangeijali, na kuiheshimu Sheria hii, furaha na amani iliyoje dunia yetu ingekuwa nayo. Mwenyezi Mungu angepewa heshima yake, uhai wa kila mtu ungelindwa kwa kicho. Jumuia leo ingekuwa tofauti sana, endapo wote wangeziangalia kwa heshima kubwa hizo Amri Kumi za Mwenyezi Mungu.
Kumi za Pekee zake Mwenyezi Mungu…
Endapo msomaji hazifahamu hizo Amri Kumi za Mwenyezi Mungu, basi, tunapenda kuiweka orodha hiyo ya sheria kumi fupi zilizotolewa kwa binadamu kutoka mbinguni. Tayari sisi tunajua kwamba Sheria hiyo ilitolewa zamani kabla ya kipindi cha Musa ilipoteremshwa juu ya vilele virefu vya Mlima Sinai. Maana Taurati yasema kwamba Ibrahimu yule ‘khalil wa Mwenyezi Mungu’ alizitii Amri za Mwenyezi Mungu.
(Taurati) Mwanzo 26:5 ‘Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.’
Hapa twamwona mmoja kutoka zile nyakati za kale aliyekuwa mwaminifu kwa Mwenyezi Mungu, yaani, ambaye alizitunza na kuziheshimu Sheria za Mwenyezi Mungu. Je, sisi tusingefuata mfano wa Ibrahimu aliyekuwa ‘hanif’? Kisha kama ukumbusho, kwa kuwa mwanadamu alikuwa amesahau, Mwenyezi Mungu alirudia kuzitaja zile Amri kwa Musa juu ya Mlima Sinai. Kutilia uzito wa umuhimu wake moyoni mwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu akaziandika Mwenyewe juu ya mbao za mawe.
Hapa chini zimeorodheshwa zile Amri Kumi kama zipatikanavyo katika: (Taurati) Kutoka 20:1-17.
“Mungu akanena maneno haya yote akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
1. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
2. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
3. Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.
4. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.
5. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.
6. Usiue.
7. Usizini.
8. Usiibe.
9. Usimshuhudie jirani yako uongo.
10. Usitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.
Hivyo ndivyo zinavyofikia mwisho wake hizo sheria fupi kumi za Mwenyezi Mungu, ambazo zimeorodheshwa pia katika (Taurati) Kumbukumbu la Torati 5:6-21. Pia zimeorodheshwa katika sehemu mbalimbali za Injili.
Msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu…
Lakini swali hili mara kwa mara laweza kuwa mioyoni mwetu na katika akili zetu, ‘je, kunatokea nini mtu akitenda dhambi’? Je, kwa Mwenyezi Mungu kuna msamaha? Mtu ye yote akitenda dhambi, na kuomba msamaha, Mwenyezi Mungu ameahidi kusamehe. Lakini, hatuna budi kumwomba, na pia kuwa tayari kutubu na kuachana na maovu. Mwenyezi Mungu atatupa sisi toba, atatupa moyo unaohuzunika hadi kufikia mahali ambapo hatutaki tena kujishughulisha na dhambi. Zingatia maneno haya kutoka katika Injili … Matendo 5:31 “Mtu huyo [Isa al-Masih] Mungu [Allah] amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi [ak-fida], awape … toba na msamaha wa dhambi.” Ni kupitia kwake Isa al-Masih aliyeteremshwa na Mwenyezi Mungu tunapata toba na msamaha wa dhambi. Isa akawa ukombozi [fidia] kwa ajili ya dhambi kwa ajili ya taifa la kibinadamu. Yeye ndiye tunu kubwa kwetu kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Hebu na tuishikilie tunu hiyo, wala tusimkatae yeye aliyeteremshwa kuja kwetu! Yatupasa tusikose kulielewa suala hili! Ni kwa njia ya Isa al-Masih sisi tunapewa msamaha! Mpokeeni Yeye!
Isa al-Masih anatupa uwezo…
Twamgeukia tena yule mtu mmoja wa watu wale wa kale aliyetoka Mashariki ambaye kama zisemavyo kumbukumbu … ali“epukana na uovu”. Ayubu 1:1 (Taurati). Aliwezaje kufanya vile? Ni kwa jinsi gani mtu ye yote anaweza kuepukana na uovu? Je, mwanadamu anao uwezo ndani yake mwenyewe wa kufanya vile? Je, mtu kwa nguvu zake mwenyewe anaweza kupigana na kumshinda Ibilisi (Shetani)? Taurati inaandika yafuatayo: Yeremia 17:5 “BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu [kuwa nguvu zake], amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake na moyoni mwake amemwacha BWANA.” Kwa mwanadamu ni kushindwa tu, hakuna tumaini katika kujitegemea wenyewe au mtu mwingine kutuokoa kutoka katika hali yetu ya kuanguka [dhambini]. Twaweza tu kuwa na tumaini tunapomwangalia Mwenyezi Mungu na Yeye aliyeteremshwa kuja hapa chini kama msaidizi wetu, yaani, Isa al-Masih!
(Injili) Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea [Isa al-Masih] aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Je, si huo uwezo ambao sisi sote tunauhitaji? Uwezo wa kushinda maisha yetu yenye dhambi! Uwezo wa kufanya mambo yaliyo ya haki! Hebu sikiliza Ewe mpendwa rafiki yake Mwenyezi Mungu, ni kwa njia ya Isa al-Masih tunapokea uwezo huo utokao kwa Mwenyezi Mungu. (Injili) 1 Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”

011:052 “Na enyi watu wangu! Ombeni msamaha kwa Mola wenu (kwa mabaya yenu yaliyopita), kisha mtubie kwake (kwa kufanya mema sasa na kuacha mabaya), atakuleteeni mawingu yateremshayo mvua tele, na atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu (mlizonazo). Wala msikengeuke kuwa waovu.” Sura 011:052 Hud

Imenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913

Maandiko ya Biblia yanatoka katika Toleo la King James (KJV)

Kwa maelezo zaidi: www.salahallah.com

“Acheni Dhambi Zilizo Dhahiri na Zilizofichikana..”

Sura 6:120
Al An-am

Mfululizo na. 09