Kiswahili 04. ‘Tukamkomboa kwa Mnyama wa Kuchinjwa Mtukufu’!

Assalamu’ alaikum

 

Kurani Tukufu inatoa mfano halisi ulio kielelezo cha utii wetu kwa Neno atokaye kwa Mwenyezi Mungu wakati Ibrahimu alipoitwa kuiacha nchi yake, jamaa zake, nyumba yake, naye akatakiwa kwenda mahali ambako Mwenyezi Mungu angemwambia. Ibrahimu alitii bila swali Mwenyezi Mungu aliponena naye. Hayo yameandikwa katika Mwanzo 12:1 (Taurati) “BWANA akamwambia Abramu [baadaye aliitwa Ibrahimu], Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonesha.” Taurati inaendelea kuandika habari za Ibrahimu alivyoitikia … Mwanzo 12:4 “Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru … Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.” Kufikia wakati huo Ibrahimu hakuwa kijana, alikuwa amejijenga, tena alikuwa tajiri, lakini Ibrahimu alipoisikia sauti yake Mwenyezi Mungu alitii pasipo shaka lo lote. Ibrahimu alikuwa hajaambiwa mahali ambako angepaswa kwenda ila aliambiwa afungashe mizigo na kuondoka, akiwa na imani kabisa kwamba Mwenyezi Mungu angemwongoza. Angalia, Ibrahimu alikuza uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, alifahamu kwamba njia yake ni bora kuliko zote, hata wakati ule alipokosa kufahamu kikamilifu kwa nini mambo yawe vile, aliliamini tu Neno lake Mwenyezi Mungu na kutii matakwa yake. Sisi nasi pia, tungetenda vema kuwa na utii ule ule aliokuwa nao Ibrahimu kwa Mwenyezi Mungu.

Ibrahimu aitwa kuchinja kafara
Kurani Tukufu yatuambia kwamba Musa alipewa Maandiko (Taurati) na kanuni ya kupambanua baina ya yaliyo ya haki na yasiyokuwa ya haki. Sura 2:53 Al Baqarah

“Na (kumbukeni) Tulipompa Musa Kitabu (kilichokusanya kila wanayoyahitajia) na cha kupambanua baina ya yaliyo ya haki na yasiyokuwa ya haki ili mpate kuongoka.” Katika Mwanzo (Taurati) kimeandikwa kisa chote cha Ibrahimu. Katika Sura ya 22 ya Mwanzo kimeandikwa kisa cha Ibrahimu alivyotakiwa kumchinja na kumtoa sadaka mwanawe. Kinatufunulia sisi jinsi yalivyotokea mambo hayo. Lakini, je, kisa hiki ni cha maana kwetu? Twaambiwa katika Sura 26:69 kwamba sisi tunapaswa ‘kusomea’ kisa chake Ibrahimu. Nabii Muhammad alijua kwamba kisa hiki kingekuwa cha maana sana kwetu kukijua, kwa maana kinalo fundisho la kutufundisha sisi. Hivyo twataka kutoa kisa chote hapa. 026:069 Ash-Shuaraa

“Na wasomee habari za (Nabii) Ibrahimu.” Katika Mwanzo 22:2 (Taurati) imeandikwa … “akasema [Allah], Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee” … halafu yanafuata maneno haya machungu mno … “umpendaye … ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
Mwenyezi Mungu alipomtaka Ibrahimu amtoe sadaka mwanawe, Ibrahimu alitii bila swali. Kisa hiki pia kimeandikwa kwa kifupi katika As-Saaffat Sura 037:102-107. Hii isingekuwa kazi rahisi kwa Ibrahimu kutekeleza! Moyo wake wenye huruma bila shaka uliumia vibaya sana zaidi ya maelezo yo yote yawezayo kutolewa. Lakini Neno kutoka kwa Mwenyezi Mungu lilikuwa limetolewa, amri ile ilisikika kwa wazi kabisa moyoni mwake na Ibrahimu alikuwa na mazoea ya kuongea na Mwenyezi Mungu. Uhusiano ulikuwa umekuzwa baina ya Mwenyezi Mungu na yeye mwenyewe kiasi kwamba aliifahamu sauti ya Mwenyezi Mungu alipoisikia. Na upendo aliokuwa nao Ibrahimu kwa Mwenyezi Mungu ulikuwa ni wa kutii alipoisikia sauti yake, hata kama alikuwa haelewi kikamilifu sababu yake ni nini.

Ibrahim aitwa ‘Hanif’
Ibrahimu anafikiriwa kuwa yeye ni ‘Hanif’ miongoni mwa wale walio wanyofu wa moyo kweli kweli na waliojitoa kumtumikia Mwenyezi Mungu. Waitwao ‘Hanif’ ni wale walio safi sana katika dini yao kwa Mwenyezi Mungu. Katika Mwanzo 22:3 tunayo maelezo kwa nini Ibrahimu anafikiriwa kuwa ni ‘Hanif’. Baada ya Ibrahimu kupewa ujumbe ule, maelezo yanasema … “Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.” Hilo ndilo linalomfanya Ibrahimu kuwa miongoni mwa ‘Hanif’. Ibrahimu aliposikia sauti ya Mwenyezi Mungu alitii na kufanya kile alichotakiwa kufanya. Je, hivi ni kweli leo kwamba wale wanaoitii sauti yake Mwenyezi Mungu, yaani, wale wanaomtii bila swali wamo pia miongoni mwa ‘Hanif’?

Ibrahimu aitwa kwenda Mlima wa Moria
Kazi hii ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amemtaka Ibrahimu kuifanya ilikuwa si mchezo. Twaweza kuona kwamba ilichukua siku tatu kwenda nchi ya Moria. Bila shaka zilikuwa siku ndefu za maumivu makali akijua kwamba huenda angerudi peke yake kutoka mahali pale pa kutolea sadaka. Twashangaa iwapo Ibrahimu alipata pumziko lo lote wakati wa usiku wengine walipolala usingizi. Kwa hakika Ibrahimu alishindana na Mungu kila usiku katika maombi juu ya jambo hilo. Twaendelea kusoma: (Taurati) Mwanzo 22:4 “Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.”
Hakuna mtu aliyepaswa kushuhudia tukio hili mbele ya Mwenyezi Mungu, zaidi ya yule baba na mwanawe. Hivyo “Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja.” Fungu la 6. Kabla ya muda mrefu kupita mwana wa Ibrahimu alisema hivi … “Babaangu … Tazama! moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.”
Wakafika mahali pale, madhabahu ikajengwa, kuni zikawekwa juu ya madhabahu, na ndipo habari zilipoelezwa waziwazi kwa mwanawe Ibrahimu ya kwamba yeye ndiye angekuwa ile sadaka. Mwanawe alitii kile Mwenyezi Mungu alichokuwa amemtaka Ibrahimu kufanya, na yule mwana akawekwa juu ya madhabahu. Huyu alikuwa ndiye yule mwana mpendwa wa Ibrahimu katika uzee wake. Ndipo Ibrahimu alipoinua juu mkono wake wenye kisu … mkono wake ule ukazuiwa…
Ibrahimu alipokuwa karibu kumchinja mwanawe, sauti ikasikika … “Ibrahimu, Ibrahimu,’ naye akasema, “Mimi hapa”. Mwanzo 22:11. Inaendelea kwenye mafungu 12-13. “Akasema [Allah], Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu [Allah], iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.”

Mwanawe Ibrahimu Akombolewa
Ni kwa njia gani mwanawe Ibrahimu alikombolewa? Kurani Tukufu yasema kwamba mwanawe alikombolewa kwa sadaka ya kuchinjwa tukufu! Sura 37:107

“Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu.” Hatuna budi kujiuliza, je, kondoo yule mume aliyenaswa katika kichaka, alikuwa “Mnyama wa Kuchinjwa Mtukufu” kweli? Au kuna habari zaidi kwa kisa hiki? Je, ingewezekana kwamba yule kondoo mume aliyenaswa katika kichaka ambaye alitolewa na Mwenyezi Mungu alikuwa akidokeza ile “Kafara Kuu”? Je, ile ilimwakilisha Yeye ambaye Mwenyezi Mungu angemteremsha kuwa sadaka ya dhambi kwa ulimwengu wote? Kwa maana yake mwanawe Ibrahimu aliwakilisha wanadamu wote. Sisi sote tungekufa milele, kama matokeo ya dhambi, lakini twaweza kuishi, kwa sababu ya mwana-kondoo mume aliyetolewa sadaka badala yetu, yaani, ukombozi ule uliotolewa na Mwenyezi Mungu. Jina lake lilikuwa Isa al-Masih, Kristo Yesu. Aliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa upatanisho kwa ajili ya wanadamu. Mwanadamu alikuwa ameanguka, lakini Mwenyezi Mungu angeweza kutoa ufumbuzi. Jamii yenye dhambi ilipaswa kukombolewa kwa kafara tukufu sana ya Yeye aliyeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ibrahimu aitwa Mbarikiwa na Mwenyezi Mungu
Kwa kuwa Ibrahimu aliitii sauti ya Mwenyezi Mungu katika jambo hili, maelezo yaliyo katika Mwanzo 22:17-18 (Taurati) yanamwita Ibrahimu kuwa amebarikiwa na Mwenyezi Mungu. Walakini si Ibrahimu peke yake aliyepaswa kubarikiwa, bali pia uzao wa Ibrahimu, hata mataifa yote ya dunia. “Katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; … na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”
Katika Mwanzo 26:5 twaambiwa tena sababu iliyomfanya Ibrahimu abarikiwe na Mwenyezi Mungu … “Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.” Baadhi ya watu watatoa hoja kwamba Amri Kumi zilikuwa hazijatolewa hadi wakati wa Musa pale Sinai, yaani kipindi kirefu baada ya Ibrahimu, lakini kisa hiki kinathibitisha milele ukweli kwamba hata Ibrahimu alizitii Amri Kumi za Mwenyezi Mungu kwa maana imeandikwa kwamba Ibrahimu alizitii Amri zake Mwenyezi Mungu.
Tukitaka kupata baraka za Mwenyezi Mungu, basi, sisi pia, sharti tupende kwa moyo kutoa utii wetu kwa Neno la Mwenyezi Mungu na kwa Amri zake, kwa njia ile ile aliyotii Ibrahimu. Kwa hakika kabisa, nasi pia tutabarikiwa na Mwenyezi Mungu.
Aya zote katika Maandiko ya Agano la Kale (Taurati) zisemazo juu ya kuchinja sadaka ya wanyama zilikusudiwa kumwongoza mtu kutazama mbele kwenye ile ‘Kafara Kuu (Tukufu)’, ya ‘Thamani Kuu’ ambayo ingeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini hatimaye Isa al-Masih alipokuja, ni wachache mno waliouelewa utume wake. Wachache mno waliamini kwamba huyu alikuwa ndiye Masihi kweli kweli, yaani, yule Sadaka ya Dhambi, Mkombozi, Mwokozi wa Ulimwengu ulioanguka dhambini.
Mmoja aweza kuuliza swali hili, kwa nini Mwenyezi Mungu alimtaka Ibrahimu aende kwenye Mlima wa Moria? Huu ulikuwa ni mlima ule ule ambao juu yake baadaye hekalu lilijengwa, lakini pia ni mahali pale pale hasa ambapo miaka mingi baadaye, Isa al-Masih, alitoa maisha yake kuwa kafara kwa ajili ya jamii yote ya wanadamu. Ilikuwa ni juu ya mlima, yaani, mlima ule ule ambapo karne nyingi kabla yake mkono wa Ibrahimu ulizuiwa ili kumwokoa mwanawe, lakini safari hii mkono wa Mwenyezi Mungu mwenyewe haukuzuiwa, na Yeye (Isa al-Masih) aliyekuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu akachinjwa kama sadaka kwa ajili ya binadamu wote. Uhai wake Isa al-Masih ulitolewa kwa ajili yetu. Yaliyompata Ibrahimu kwa mwanawe, lilikuwa ni fumbo linaloonesha yale ambayo yangekuja baadaye. Katika siku zake Ibrahimu, ukombozi ulipatikana, yaani, yule kondoo mume kichakani. Katika Injili, inasema … “Kama vile Mwana wa Adamu … [alivyokuja] kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mathayo 20:28).
Hapo kale, watu wale wenye hekima kutoka Mashariki walijua kwamba ukombozi ungekuja kwa ajili ya wanadamu. Katika Vitabu Vitakatifu twasoma haya yafuatayo: … “Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi” Ayubu 33:24.
Ukombozi ni gharama inayolipwa kwa ajili ya mwenye dhambi ili apate kusamehewa dhambi zake. “Mshahara wa dhambi ni mauti’, na ilimpasa mtu fulani kulipa gharama hiyo kwa ajili ya mwanadamu, vinginevyo, yeye kwa hakika angetazamia tu kushuka shimoni [kwenye maangamizi], imeandikwa katika Injili, kwamba Mwenyezi Mungu alitoa sadaka ya dhambi, yaani, ukombozi … Waebrania 10:12 “Lakini huyu (Isa al-Masih), alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu [Allah]”.
1 Yohana 2: 2 “Naye (Isa al-Masih) ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.”
Mpendwa rafiki wa Mwenyezi Mungu, je, hutaipokea sadaka hii ya dhambi, yaani, ukombozi huu ulioteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili yako? Mpendwa rafiki, ni kwa ajili yako Mwenyezi Mungu alimteremsha Isa al-Masih, yule Masihi kama “Mnyama wa Kuchinjwa Mtukufu”. Ameteremshwa kwako wewe na kwangu mimi, kama Mwokozi wetu kutoka dhambini. Tafadhali ipokee leo hii dhabihu hii iliyotolewa kwa neema kwa ajili yako!

Aya za Kurani zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913

Aya za Maandiko/Biblia zimetolewa kutoka Toleo la King James (KJV)
www.salahallah.com
Tukamkomboa
Kwa Mnyama
Wa
Kuchinjwa
Mtukufu’
Sura 37:107
As-Saaffat

Mfululizo na. 04