Kiswahili 33. “Nguo za Utawa [Zifunikazo]” sehemu ya pili

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!
Salamu katika jina lake Mwenyezi Mungu awekaye juu yetu vazi lifunikalo la ‘Haki’. Na ubarikiwe uwe na vazi hilo. Kurani Tukufu yatuambia… “Enyi wanaadamu! Hakika tumekuteremshieni nguo zifichazo tupu zenu na nguo za p ambo, na nguo za utawa (yaani, kucha Mungu) ndizo bora. Hayo ni katika Ishara za (neema za) Mwenyezi Mungu ili wapate kukumbuka.”
Sura 7:026 Al Aaraf
Kurani Tukufu inasema juu ya nguo zifunikazo za aina mbili… ya kwanza ni nguo zifunikazo zilizotengenezwa na wanadamu kuficha aibu yetu na utupu wetu… Hii ndiyo aina moja ya nguo zifunikazo au vazi. Walakini, nguo hizo hazitoshi katika hukumu ile. Kule tunahitaji vazi lifunikalo la aina nyingine lililo bora… Vazi lifunikalo la ‘haki’. Ni kwa vazi pekee lifunikalo la ‘haki’, yaani, hili la pili, ambalo sisi tutapewa, tutaweza kuingia katika ufalme wa Mbinguni.

 

Kwa nini vazi hili la Haki ni la muhimu sana? Vazi hili la pili lifunikalo linaakisi tabia ya Mungu. Vazi hili la pili ni la mwisho, lakini ni bora. Lilipotezwa katika Bustani ya Edeni wazazi wetu wale wa kwanza walipoanguka kwa kuusikiliza uongo wa Ibilisi. Ili kurudi katika ufalme wa Mungu ambao kutoka katika huo mwanadamu alianguka, anahitaji ‘haki’, ambayo ni kuishi maisha mema na kuwaza mawazo safi, kwa kifupi… “Dini ya Kweli.” Mwenyezi Mungu kwa fadhili zake nyingi alikuwa amempa mtu yule wa kwanza na mkewe uthibitisho mwingi wa wema kwa kumpa yule mume na mkewe mahali kama pale papendezapo katika ile Edeni ya Mungu. Kila mti uliozaa matunda ulikidhi mahitaji yao na yale yote ambayo yangefanya maisha yao kuwa ya furaha na yapendezayo walipewa. Hivyo upendo wa Mwenyezi Mungu ulionekana pande zote ukiwazunguka.
Kwa upande mwingine, Ibilisi alikuwa hajawapa uthibitisho wo wote wa upendo wake kwao wala hakuwapa mahitaji yao, lakini maneno yake yalipokewa upesi na kusadikika kuliko lile Neno la Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo, mume yule na mkewe waliokuwa watakatifu, walivyoanguka kutoka katika hali yao ya juu walipokula tunda lile lililokatazwa. Wakaipoteza ile haki, yaani, lile vazi zuri lililowafunika walilokuwa wamepewa, walipoacha kumwamini Mungu.

Haki ni kitu fulani kinachotokea ndani ya moyo wa muumini. Tangu anguko lile la mwanadamu, haki ni kitu fulani kisichoweza kutokea kwa juhudi za kibinadamu. Hata wale wasioamini wanaweza kutoa sadaka zao kwa maskini (zakat), na hilo ni jema sana, wanaweza kutenda matendo mengi ya huruma, lakini hayo yaweza kuwa ni mtindo wa haki kwa kuonekana nje na pasiwe na nia halisi kutoka moyoni iwezayo kuwasukuma. Mengi hutendwa kwa madhumuni ya kujionesha kwa watu… ili watu waweze kukusifu kwa wema wako. Hii siyo haki. Hili lilikuwa tatizo huko nyuma katika siku zake Isa [Yesu]. “Tena matendo yao [Wayahudi] yote huyatenda ili kutazamwa na watu…” Injili Mathayo 23:5.

Hata leo hii waumini wanaweza kusema sala zinazorudiwa mara nyingi, ambazo wamezikariri, mara tano kwa siku… walakini hilo linaweza kuwa tendo lifanyikalo bila kufikiri. Ni karibu sana sawa kama mashine… ni kama kumbukumbu iliyorekodiwa, unabonyeza tu swichi, nawe unaisikia sala ile ile… je! hivi hayo ndiyo atakayo Mwenyezi Mungu? Yaani, sala zetu zilizorekodiwa? Bila shaka kuna jambo fulani lenye kina zaidi litakiwalo, pengine sala zetu hazina budi kutoka ndani ya mioyo yetu. Mimi nimebahatika kuwa na watoto na wanapoongea nami kutoka moyoni mwao, naweza kuyathamini sana wasemayo. Waniambiapo kwamba wananipenda, moyo wangu unasisimka. Lakini endapo wangerekodi upendo wao huo kwenye Sidi na kupiga ujumbe huo uliorekodiwa mara nyingi ili nisikilize, moyo wangu usingeguswa hata kidogo. Bila shaka kwa kiasi fulani huenda hilo likafanana na wakati ule tunapomkaribia Mungu. Maongezi yetu pamoja naye ni sharti yatoke ndani yetu na kusemwa kwa moyo wenye shukrani.

Je, hivi kuna jambo fulani litokealo moyoni Mwenyezi Mungu anapotugusa ndani yetu?

Haki ya kweli ni wakati ule matendo mema yatokapo ndani kabisa ya moyo wa mtu. Matendo kama vile… kukataa kulipiza kisasi na kumrudishia mtu fulani anapotukosea. Matendo kama kuwatendea mema maadui zako, kuwa na huruma moyoni mwako… ukikataa kumwumiza mtu fulani aliyekuchukiza sana unapokuwa na uwezo kumdhuru. Kuwa na sala (dua) za faragha kwa ajili ya wale wanaokutesa. Ni Mungu peke yake awezaye kutupa sisi haki ya jinsi hii. Kwa mwanadamu hilo haliwezekani. Ni zawadi kutoka Mbinguni kupitia yule aliyeteremshwa aitwaye Masihi Isa. Tunahitaji watu watakaoomba sana kuwa na utakatifu huu moyoni. Tena yaja ahadi hii kutoka kwa wakuu wale wa Zamani wa Mashariki, ambayo wewe waweza kudai kama yako mwenyhewe.
“Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia; hata auone uso wake kwa furaha; Naye humrejezea mtu haki yake.”
Ayubu 33:26 Toleo la Kisasa la King James

Mwenyezi Mungu ameahidi kurejeza kile kilichopotea kule Edeni! Enyi rafiki zangu, hizi ni habari njema zenye nguvu… ingawa sisi tumeanguka na kuwa na makosa, bado hatujaachwa. Twaweza kurejezewa tabia ya Mwenyezi Mungu! Yeye ni mwema kwa wasio na shukrani. Anawajali makafiri, akiwapa jua na mvua, vidonda vyao anaviponya… Wasio na shukrani wanacho chakula, mavazi na mahali pa kulala. Mwenyezi Mungu hutoa wokovu kwa wasio haki. Atatufunika tena na vazi lake la Haki. Je, twayasadiki hayo? Hii maana yake ni kuwa na “dini ya kweli” si ule mfano wake tu, bali yenyewe hasa. Kitu fulani cha kweli kitokacho moyoni na kuonekana katika maisha ya kila siku! Hilo likitokea, basi, mfumo wa dua zetu huwa tofauti kabisa. Hatuwi tena na dua zilizorekodiwa ambazo twazisema kwa sauti ya chini na kuharakisha kana kwamba tunatimiza wajibu fulani, lakini itikio litokalo moyoni huonesha Mwenyezi Mungu alivyo wa maana kwetu. Rafiki zangu, je! hayo ndiyo mnayotamani moyoni mwenu? Mwaweza kuwa nayo na yatatolewa kwenu bure! Yote haya hupitia zawadi ya ‘Mwana Mwenye Haki’ aliyeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sura 19:10 Maryam.
Hii ndiyo hali ya kila mtu… “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.” Warumi 7:18
Lakini kama Ibrahimu sisi twaweza kuziamini ahadi… “[Ibrahimu] akamwamini BWANA, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.” Taurati Mwanzo 15:6
Bila kujali kasoro walizo nazo watu wa Mungu, Kristo hawapi kisogo watu wake anaowajali. Anao uwezo wa kuyabadilisha mavazi yao. Anaondoa mavazi machafu [uchoyo wote na dhambi], anaweka juu ya wale wanaotubu na kumwamini vazi lake mwenyewe la Haki, na kuandika msamaha mbele ya majina yao katika kumbukumbu za mbinguni. Anawakiri mbele ya ulimwengu wa mbinguni. Ibilisi, adui yao, anadhihirishwa kuwa ni mshitaki wao na mdanganyaji. Mwenyezi Mungu atatenda haki kwa wateule wake. Mungu wetu asema…
“Mvueni [huyo mwenye dhambi] nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi …” Zekaria 3:4,5.
Hata hivyo, Mungu atakufunika wewe na ”vazi la haki.” Isaya 61:10.

Kumbuka kwamba vazi hili la haki ni ishara itokayo kwa Mwenyezi Mungu… “Na nguo za utawa (yaani kucha Mungu) ndizo bora. Hayo ni katika Ishara za (neema za) Mwenyezi Mungu…” Sura 7:026 Al Aaraf

Hakika vazi hili au kifuniko hiki cha Mwenyezi Mungu ni ile Haki yake Kristo, yaani, tabia yake mwenyewe isiyo na waa, ambalo kwa imani hutolewa kwa wote wanaompokea yeye kama Mwokozi wao kila mmoja binafsi.

Lile vazi jeupe la utakatifu lilivaliwa na wazazi wetu wa kwanza walipowekwa na Mungu katika Edeni takatifu. Waliishi kikamilifu kulingana na mapenzi yake Mungu. Nuru nzuri ambayo mwanga wake ulififia, yaani, nuru ya Mungu iliwazunguka, mume yule na mkewe, ambao walikuwa watakatifu. Vazi hili la nuru lilikuwa ishara ya mavazi yao ya kiroho ya utakatifu wao wenye asili ya mbinguni.. Laiti kama wangalidumu kuwa wanyofu kwa Mungu lingeendelea daima kuwafunika. Walakini dhambi ilipoingia, walikata kiungo chao kilichowaunganisha na Mungu, na ile nuru iliyokuwa imewazunguka ikaondoka. Wakiwa uchi na wakiona aibu, walijaribu kushona majani ya mtini kujifunika ili yawe badala ya mavazi yale ya mbinguni.

Hakuna cho chote awezacho kubuni mwanadamu kiwezacho kuchukua mahali pa vazi lake la utakatifu lililopotea. Ni vazi lile tu lifunikalo ambalo Kristo mwenyewe ametoa laweza kutufanya sisi tufae kuonekana mbele zake Mungu. Vazi hili lifunikalo, yaani, vazi la haki yake, Kristo ataliweka juu ya kila mtu atubuye na kuamini. “Nakupa shauri,” anasema, “ununue kwangu… mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekanwe.” Ufunuo 3:18. Anasema, “ununue”, yaani, litakugharimu kila kitu ili kulipata, lakini lenyewe linatolewa bure.
Vazi hili, lililofumwa katika kiwanda cha mbinguni, ndani yake halina hata uzi mmoja uliobuniwa na mwanadamu. Katika ubinadamu wake Kristo alikuwa na tabia kamilifu, na tabia hii anajitolea kutugawia sisi. “Matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi.” Isaya 64:6
Kila kitu tuwezacho kufanya sisi wenyewe kimechafuliwa na dhambi. Lakini Mwana wa Mungu “alidhihirishwa ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.” Dhambi inafafanuliwa kuwa ni “uvunjaji wa sheria.” 1 Yohana 3:5,4.
Haki yake Kristo haitafunika dhambi moja inayopendwa sana moyoni.

Ni kile tu kipatanacho na kanuni za sheria ya Mungu kitakachosimama hukumuni.

Hapo baadaye hapatakuwapo na nafasi nyingine ya kujitayarisha kwa umilele. Ni katika maisha haya tunatakiwa kuvaa vazi la haki yake Kristo. Hii ndiyo nafasi pekee kwetu ya kujenga tabia kwa ajili ya makao yale aliyowaandalia wale wanaozishika amri zake. Siku za muda wetu wa kujaribiwa [kupimwa] zinaharakisha sana kuisha. Mwisho ule u karibu. “Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.” Ufunuo 16:15.

Wapendwa rafiki zangu, hatuna muda wa kuchelewa-chelewa na kulipuuzia somo hili muhimu. Sasa ndio wakati wa kusali na kusihi kwa dhati ili Mwenyezi Mungu atupe sisi mbaraka huo. Msifanye kosa, kukosa hapa ni kukosa umilele. Mwenyezi Mungu na atupe ishara yake… yaani, Vazi la Haki.
Kwa maelezo zaidi juu ya somo hili na mengineyo, tafadhali tembelea tovuti yetu chini. Maswali yako au maoni yako yanakaribishwa sana!

www.salallah.com

“Vazi la Haki”
Sehemu ya Pili

Sura 7:26
Al Aaraf

Mfululizo na.33