Kiswahili 37. “Ibrahimu, Imamu wa Mataifa”

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!

 

Ibrahimu alikuwa mtu mkuu wa Mwenyezi Mungu. Aliheshimiwa sana na Mungu, tena alichaguliwa kuwa kielelezo au mfano wa kufuatwa na wengine.
Yeye anaitwa “Imamu wa Mataifa” katika Kurani Tukufu. Twatamani kuyachunguza maisha ya mtu huyu mashuhuri aliyechagua kumfuata Mungu huku ukiwapo uwezekano mkubwa kwake wa kufaulu au kushindwa. Inaelezwa katika Kurani Tukufu kwamba baba yake mwenyewe alimpinga na kuna mwelekeo mkubwa sana kwamba ndugu zake wengine walimpinga pia. Kumfuata Mungu bila ya masharti kwa upande wetu kila mara kunakuwa na gharama. Mara nyingi hawatatuelewa vizuri wale watuzungukao na hasa wale wa familia yetu au umma wetu. Mtu fulani anayemfuata Mungu kwa karibu sana ataangaliwa na watu kama mtu wa ajabu, kwa maana kuifuata sauti ya Mungu kwaweza kutuleta katika mgongano na hata wale wa dini yetu.

“Na (kumbukeni khabari hii:) Mola wake alipomfanyia mtihani (Nabii) Ibrahim kwa amri nyingi; naye akazitimiza. Akamwambia: ‘Hakika mimi nitakufanya Kiongozi [Imamu] wa watu (wote).’ (Ibrahim akasema:) ‘Je, na katika kizazi changu pia?’ Akasema: ‘Ndio lakini) ahadi Yangu haitawafikia (waovu) madhalimu wa nafsi zao’; (itawafikia walio wazuri)’.” Sura 2:124 Al Baqarah

Twataka kumwangalia mara nyingine tena huyo “Imamu wa Mataifa”, kuona aliishi miaka mingapi. Tunayo picha itokayo katika Vitabu Vitakatifu Taurati na Injili ioneshavo jinsi Ibrahimu alivyoenenda katika maisha yake. Kutoka katika vyanzo hivi sisi twaweza kupata mtazamo bora kwa nini Mwenyezi Mungu alimwita Imamu, Kiongozi wa wale wamtafutao Mwenyezi Mungu kwa moyo wao wote.

“Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.” Taurati Mwanzo 18:19
Hata makafiri walioishi wakati wa Ibrahimu walitambua ya kuwa Mungu alikuwa pamoja naye.
“Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda.” Taurati Mwanzo 21:22

Je! hivi ni dhahiri kwa makafiri wa leo kujua Mungu yu pamoja nawe na yu pamoja nami? Kama makafiri hawawezi kuona hilo, je, ni kwa sababu sisi tunashindwa kuunganika na Mungu itupasavyo?

Kielelezo cha Ibrahimu
Kuna vielelezo mbalimbali katika maisha yake Ibrahimu ambavyo yatupasa kuviangalia na ambavyo sisi tungeviangalia kama mfano kwetu wa kuiga. Ibrahimu alikuwa na mtazamo wa unyenyekevu sana kuhusu yeye mwenyewe…
“Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu.” Taurati Mwanzo 18:27

Taurati yasema hivi juu yake, “…Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.” Taurati Mwanzo 26:5

Eneo moja ambalo twatamani kuliangalia lilikuwa ni eneo lile la ukarimu wa Ibrahimu. Mtindo wake wa kumrudishia Mwenyezi Mungu utajiri wake. Kama lilivyo jambo hilo hivi leo, kwa mara nyingi sana, matajiri wamekuwa hivyo kwa sababu ya kuhodhi mali, hii ndiyo maana wao ni matajiri, walakini, Ibrahimu hakuhodhi mali kwa ajili yake binafsi. Kwa ukarimu alimrudishia Mungu sehemu ya kumi ya ongezeko la mali yake. Naam, ni jambo lisilosadikika kama lilivyo, huo ndio mfano ambao hautiliwi maanani na waumini. Wanaridhika kutoa asilimia ndogo zaidi, yaani, asilimia 2 au 3 ya mapato yao, wanasema hiyo inatosha, lakini, je, Taurati yasemaje juu ya kiwango ambacho Ibrahimu alimrudishia Mungu. Wakati uliopita Mwenyezi Mungu aliwajulisha watu kupitia wale manabii wa mwanzo kile anachotarajia kupata kutoka kwa watu wake na kile anachotaka sisi tumrudishie yeye. Mfano huo uliowekwa tangu zamani ndio Ibrahimu na wengine waliufuata wakimpa Mungu kwa moyo wa hiari. Huo ndio mfano wetu pia.
“Tena zaka yote ya ng’ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa BWANA.” Mambo ya Walawi 27:32
Hapa kwa lugha isiyoweza kukosewa ambayo hakuna awaye yote awezaye kukosea, yatuambia sisi ya kwamba Bwana alitarajia kupewa “zaka” au “sehemu ya kumi” ambayo ndiyo maana ya “zaka”. Yaendelea kusema hivi katika Taurati:
“Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; ni takatifu kwa BWANA.” Mambo ya Walawi 27:30

Tunao ushauri huo uliofuatwa na Ibrahimu muda mrefu kabla ya wakati huu. Kumbukumbu yasema kwamba Ibrahimu alitoa sehemu ya kumi au zaka kwa kuhani wa Mungu, Melkizedeki.

“Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako.” Abramu [Ibrahimu] akampa fungu la kumi la vitu vyote.” Taurati Mwanzo 14:20

Tendo hilo lilikuwa la maana sana ambalo Ibrahimu alilitenda kiasi kwamba liliandikwa tena miaka mingi baadaye katika Injili. “Bali yeye [Melkizedeki]; ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi.”
Injili Waebrania 7:6

Mwenyezi Mungu auliza Swali!
“Je! mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu [sadaka].” Malaki 3:8

Hapo kale watu wake Mwenyezi Mungu walimwibia kwa kukataa kumrudishia zaka au sehemu ya kumi. Waliitumia wenyewe, na kujifanya matajiri, lakini tendo hilo lilifikiriwa kuwa ni kumwibia Mungu.

Jambo hilo lipo hata leo. Mwenyezi Mungu ametupa utajiri wake kwa wingi, naye anataka sisi tumrudishie sehemu ya kumi ya ongezeko tupatalo na juu ya hiyo tutoe sadaka. Hapo kale wale waliokuwa waaminifu katika Israeli walitoa asilimia ishirini au hata zaidi kwa ajili ya kazi ya Mungu. Leo hii sisi kama watu tuishio mwisho wa kufungwa historia ya ulimwengu huu yatupasa kulizingatia hilo kwa makini sana na kuuiga mfano huo. Je, haitupasi kuwa wacha Mungu zaidi na kuwa tayari kutoa kwa moyo kama wao walivyofanya. Kitu cho chote kilicho pungufu ya hicho kwa kweli ni wizi tena ni kuzuia kile ambacho kwa haki ni chake Mwenyezi Mungu.

Maisha ya Ibrahimu yalikuwa ya ukarimu kadiri alivyozidi kujitahidi kuwa katika amani na Mbingu. Roho ya ukarimu ni roho ya mbinguni. Mbingu ina roho ya kutoa, na roho hiyo inajidhihirisha sana ndani ya Masihi Isa katika kafara yake kuu kuliko zote aliyoitoa pale msalabani. Kwa ajili yetu sisi Mwenyezi Mungu alimtoa Mwanawe pekee, na Kristo, alipokwisha toa vyote alivyokuwa navyo akajitoa nafasi yake, ili mwanadamu apate kuokolewa. Kilichotendeka juu ya ule Mlima Moria miaka elfu mbili iliyopita huonesha kwa lugha isiyo na kifani kwamba Mbingu ilitoa kilicho bora kabisa kwa ajili ya wanadamu ili kutukomboa na kutulipia fidia tusikabiliwe na mauti ya milele. Tukio lile kuu, Isa alipotoa uhai wake kwa ajili ya wanadamu wote lingemgusa kila mtoto wa Mwenyezi Mungu kuwa na moyo wa ukarimu. Kwa upande mwingine, roho ya uchoyo ni roho ya Ibilisi au Shetani. Kanuni inayoonekana katika maisha ya wale waipendao dunia hii ni kupata, kupata. Hivyo wao wanatumainia kujipatia furaha na raha, lakini tunda lao walilolipanda linawaletea taabu na mauti. Mpaka hapo Mungu atakapoacha kuwabariki watoto wake ndipo nao watakapofunguliwa vifungo vya kumrudishia sehemu yake anayodai apewe.

Madai ya Mwenyezi Mungu ya zaka yetu au sehemu yetu ya kumi
“Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.” Malaki 3:10-11

Mwenyezi Mungu anatutaka sisi tumjaribu au tumpime. Ili sisi tuweze kufanya hivyo, ni lazima tumwamini kama yeye asemavyo. Mimi ningependekeza sana kwamba msomaji azithibitishe ahadi hizo za Mwenyezi Mungu kuona kama ni za kweli! Mrudishie zaka au sehemu ya kumi ya ongezeko la mapato yako na kuona kama madirisha yatafunguka au milango ya mbinguni haitafunguka kwa ajili yako! Ahadi ni kwamba hapatakuwa na nafasi ya kutosha kuiweka mibaraka hiyo. Pia yeye anaahidi kuyalinda mali yetu na mashamba yetu yasiharibiwe. Mimi nimekwisha kumjaribu Mwenyezi Mungu katika jambo hilo, nami naweza kusema kweli ya kuwa ninavyo vingi zaidi kuliko niwezavyo kuvibeba! Mibaraka yake inavizidi vile ninavyomrudishia yeye.

“BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.” Kumbukumbu la Torati 28:8

Wapendwa rafiki zangu, je, mngependa Mwenyezi Mungu aamuru baraka ije juu yenu? Hivi ndivyo isemavyo na hivi ndivyo atakavyofanya kama tutatekeleza masharti… je, hivi mko tayari kutii na kumrudishia sehemu ya kumi? Basi msiogope kumwomba mibaraka ambayo Mwenyezi Mungu ataiamuru ije juu yenu!

Je, rafiki zangu, hazina yenu iko wapi? Masihi Isa anaielezea hivi kanuni hii. “Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.” Injili Mathayo 6:21

Rafiki zangu, sisi tungebarikiwa endapo tungefuata mfano wa Ibrahimu, Imamu wa Mataifa, wa kumrudishia Mwenyezi Mungu sehemu ya kumi ya ongezeko la mapato yetu.

Unabii wa wakati wa mwisho
Tamati yake kuna unabii mwingi wa zamani wa Isaya 60 ambao unawajumuisha Wana wa Mashariki (Islamu ya leo) katika mkao wa siku za mwisho pamoja na uhusiano wao na Mwenyezi Mungu na watu wake wale walio waaminifu wa kile Kitabu. Watu hao wataleta utajiri wao na kumletea utukufu Mwenyezi Mungu na kuufanya usonge mbele ujumbe wa siku ya mwisho kabla dunia hii haijafikia mwisho wake na kabla Isa hajarejea. Mpendwa, rafiki yake Mwenyezi Mungu, anakutaka wewe ufanye sehemu yako katika kazi yake ya mwisho humu duniani. “Wingi wa ngamia utakufunika, ngamia vijana wa Midiani na Efa; wote watakuja kutoka Sheba; wataleta dhahabu na uvumba; na kuzitangaza sifa za BWANA. Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako, kondoo waume wa Nebayothi watakutumikia; watapanda juu ya madhabahu yangu kwa kibali, nami nitaitukuza nyumba ya utukufu wangu. Ni nani hawa warukao kama wingu, na kama njiwa waendao madirishani kwao? Hakika yake visiwa vitaningojea, na merikebu za Tarshishi kwanza, ili kuleta wana wako kutoka mbali, na fedha yao na dhahabu yao pamoja nao, kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wako, kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli, kwa kuwa amekutukuza wewe. Na wageni watajenga kuta zako, na wafalme wao watakuhudumu; maana katika ghadhabu yangu nalikupiga, lakini katika upendeleo wangu nimekurehemu.” Taurati Isaya 60:6-10.
www.salahallah.com

“Ibrahimu, Imamu wa Mataifa”

Sura 2:124
Al Baqarah

Mfululizo na.37