Kiswahili 08. Kitabu cha Mwenyezi Mungu

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

 

Je, Biblia ni Neno lake Mwenyezi Mungu?
Je, Biblia yaweza kutegemewa? Je, hilo ni Neno litokalo kwake Mwenyezi Mungu? Haya ndiyo maswali ambayo mara kwa mara tunaulizwa na watu wengi siku hizi, hata na Waislamu wanauliza swali hili muhimu.
Hivi twawezaje kufahamu? Je, Maandiko ya Biblia yameteremshwa kweli kutoka kwa Mwenyezi Mungu? Kabla hatujatafuta majibu namwomba msomaji apeleke dua yake kwa Mwenyezi Mungu, kwa maana Mwenyezi Mungu ajua vizuri sana. Yeye atatoa jibu ambalo watu walio wa kweli wanauliza kwa moyo mnyofu ulimwenguni kote! Sikuzote Mwenyezi Mungu atajibu maswali yaliyoulizwa kwa moyo mnyofu kama hilo iwapo ombi linatoka katika kilio cha kweli cha kuijua ile kweli.
Wakati mwingine twaweza kupata majibu ya swali kwa kuuliza swali jingine, ‘Je, Nabii Mstahiki Muhammad alivionaje Vitabu Vitakatifu vya Maandiko ya Biblia’? Alilijibuje swali hili mtu huyu Mstahiki kuhusu “Taurati” na “Injili” [Maandiko ya Biblia]? Tunamwomba msomaji kuigeukia Kurani Tukufu na kuzipata aya zifuatazo:
Sura 2:53

002:053 “Na (kumbukeni) Tulipompa Musa Kitabu (kilichokusanya kila wanayoyahitajia) na cha kupambanua baina ya yaliyo ya haki na yasiyokuwa ya haki ili mpate kuongoka.” 2:053 A.-Baqara

Sura 3:3 “Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati [ya Musa] na Injili. [ya Yesu]. Zamani – ziwe uongozi kwa watu. Na akateremsha vitabu vingine vya kupambanua baina ya haki na batili. 003:003[-004] Aali Imran
Kurani Tukufu inataja kanuni moja tu ya kupambanua katika Hukumu, na hiyo ni Maandiko Matakatifu, Taurati. Katika Taurati tunauona msingi wa Hukumu, uitwao Amri Kumi. Huu ndio msingi wa serikali ya Mbinguni. Unapatikana katika (Taurati) Kutoka sura ya 20:1-17.

021:048 ‘Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haruni (kitabu kilicho) kipambanuzi na mwanga na mauidha kwa wacha – Mungu.’ 21:048 Al-Anbiyaa
Kurani Tukufu yatuambia kwamba Taurati ni Mwanga na Mauidha (Ujumbe) kwa wacha–Mungu. Anathubutuje, basi, mtu awaye yote kuyadharau mauidha haya? Je, lisingekuwa jambo la kutisha kutoa mawazo yasemayo kwamba Taurati si Neno lake Mwenyezi Mungu?

Sura 10:094 “Na kama unayo shaka juu ya hayo tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao vitabu [Maandiko ya Biblia] kabla yako (Myahudi na Manasara wale waliosilimu). Kwa yakini haki imekwisha kukujia kutoka kwa Mola wako, kwa hiyo usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka.” Sura 010:094 Yunus
Hapa katika aya hii Mstahiki Muhammad amewaambia wasomaji “kuwauliza” wale ambao wamekuwa wakisoma Kitabu (Maandiko ya Biblia) kabla yao. Kwa nini Nabii huyu Mstahiki anayaelekeza mawazo yetu kwa wale wanaoiheshimu Biblia, isipokuwa kama alijua tu kuwa walikuwa sahihi?

Sura 005:044
‘Hakika tuliteremsha Taurati yenye uongozi na nuru; ambayo kwayo Manabii waliojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu) waliwahukumu Mayahudi: na watawa na maulamaa pia (walihukumu kwa hiyo Taurati), kwa sababu walitakiwa kuhifadhi Kitabu (hicho) cha Mwenyezi Mungu; nao walikuwa mashahidi juu yake. Basi (ninyi Waislamu) msiwaogope watu, bali niogopeni (mimi). Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache (ya duniani). Na wasiohukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.’ Sura 005:044 Al Maidah

Hizi ni baadhi tu ya sura nyingi zilizoorodheshwa katika Kurani Tukufu zishuhudiazo kuwa Taurati na Injili viliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni kwa ajili ya watu wote (Binadamu). Hapa hata inaiita Taurati kuwa ni “Kitabu cha Mwenyezi Mungu”.

Baadhi ya watu wangependa kutoa hoja zao kwamba Biblia imebadilishwa na kuchafuliwa, yaani, kwamba haiwezi kutegemewa tena? Kwa usemi huo, twauliza swali rahisi. Kama Biblia ilikuwa imebadilishwa kabla ya kipindi cha Muhammad kwa kiwango ambacho isingeweza kutegemewa tena, basi, kwa nini Nabii huyu Mstahiki aliyaelekeza sana mawazo ya watu kwenye [kitabu] hicho? Je, Mwenyezi Mungu angemwelekeza Nabii huyu Mstahiki kwenye kitabu hiki cha uongo kilichochafuliwa? Hasha! hili huonesha tu kwamba Maandiko ya Biblia yaliaminika katika kipindi kile cha Muhammad.
Hivyo, basi, endapo Maandiko ya Biblia yangekuwa yamechafuliwa tangu kipindi kile cha yule Nabii Mstahiki, basi yako wapi maandiko ya mkono ambayo ni ya kweli? Hakuna hata mmoja aliyeweza kuonesha maandiko ya mkono kama hayo kwa sababu hayako. Maandiko ya Biblia yale yale yaliyokuwako wakati wa Muhammad ndiyo yale yale ambayo bado yanapatikana leo. Kumbuka kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuyahifadhi Maneno yake yasichafuliwe ili mwanadamu leo apate kuyajua Mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Zaidi ya haya yote, nani angeweza kufanya kazi ngumu ya kuyatafuta maandiko yote ya mkono ya Biblia na kuyakusanya pamoja ili kuyabadilisha au kuyafanya ya uongo? Fikiria kwa makini sana juu ya jambo hili mpendwa msomaji!
Mauidha yaliyo katika Injili bado yanadumu kuwa ya kweli leo. (Injili) Mathayo 4:4 ‘Yesu [Isa al-Masih] akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu, (ila kwa kila neno la Mungu (Allah).’
Kwa salama sisi twaweza kuliamini Neno lake. Ninao ushuhuda wangu binafsi kuhusu kile Neno la Mwenyezi Mungu, yaani, Biblia, lilichonifanyia mimi. Kujifunza Kitabu hiki hubadilisha maisha. Katika kurasa za Kitabu hiki (Maandiko ya Biblia) umo uwezo, yaani, nguvu inayotolewa kwa wale wanaotumia muda wao kufahamu yaliyomo. Mabadiliko yanaonekana dhahiri. Kwake yeye anayetii Maneno haya ya Mwenyezi Mungu atagundua kwamba mtu anapata mwonjo mpya, mawazo mapya, hisia mpya, makusudi mapya yatakayoyaongoza maisha yake. Haya yote hutokea unapomtii Mwenyezi Mungu na Neno Lake aliloliteremsha hapa chini.
(Injili) Yohana 6:63 ‘Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima’. Isa al-Masih alisema waziwazi ya kwamba maneno hayo ni ‘roho’ na tena ni ‘uzima’.
Wenye hekima kutoka Mashariki wa zama za kale waliiona thamani ya Neno lake Mwenyezi Mungu. (Taurati) Ayubu 22:22 “Uyapokee, tafadhali, mafunzo (Taurati) yatokayo kinywani mwake, na maneno yake yaweke moyoni mwako.’
Tena Ayubu mtu yule mwenye hekima wa zamani anatuambia sisi kwamba … “Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu.” (Taurati) Ayubu 23:12.
Hatuhitaji kuwa na hofu kwamba Neno la Mwenyezi Mungu lingeweza kuchafuliwa. Je, Mwenyezi Mungu si anao uwezo usio na kikomo? Je, hawezi kutegemewa kuwa atalihifadhi Neno lake leo kwa ajili yetu hapa duniani? Ikiwa Mwenyezi Mungu anaweza kuzihifadhi nyota zinazozunguka katika ukanda wake na kuhifadhi mamilioni yasiyohesabika ya nyota zinazokwenda kwa kasi mbalimbali zisigongane, basi, ni jambo rahisi jinsi gani kwamba Yeye pia aweze kulihifadhi Neno Lake aliloliteremsha chini, likiwa kamili kabisa. Ni kweli hili ni jambo rahisi kwa Mwenyezi Mungu.

Sura 6:115
‘Na yametimia maneno ya Mola wako kwa kweli na uadilifu. Hakuna awezaye kuyabadilisha maneno Yake. Na Yeye ndiye asikiaye (na) ajuaye.’ 6:115 Al An-am
Kwa bahati mbaya wengi wamelitangua Neno la Mwenyezi Mungu kwa mapokeo waliyopokea yasiyo na msingi wo wote katika vile Vitabu Vitakatifu. Tunahitaji kuwa waangalifu sana mauidha haya yasije yakatuhusu na sisi … (Injili) Marko 7:13 “Huku mkilitangua Neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.’ Maneno haya ya onyo yatokayo kwa Isa al-Masih yanatuhusu sisi pia kama wale wa siku zile. Hebu na tulizingatie onyo hilo. Siku ile itakuwa ya kutisha jinsi gani tukijikuta tumeyatangua Maneno ya Mwenyezi Mungu!
Rafiki zangu, sasa kuliko wakati mwingine wo wote uliopita ni wakati wa kulizingatia kwa njia ya pekee lile Neno lililoteremshwa kwetu (Taurati na Injili). Kila siku maneno yake yazame ndani kabisa ya mioyo yetu. Mwenyezi Mungu na ayabadilishe maisha yenu ili ninyi pia mweze kutoa ushuhuda kwamba kweli haya ni Maneno yatokayo kwa Mwenyezi Mungu … na ya kwamba yanaweza kututayarisha sisi kukabiliana na siku za usoni bila ya kuogopa.
(Injili) 2 Timotheo 3:16-17 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”
(Taurati) Isaya 40:8 “Majani yakauka, ua lanyauka; Bali Neno la Mungu [Allah] wetu litasimama milele”.
Neno La Mwenyezi Mungu kama lilivyoandikwa katika Taurati na Injili ndicho “Kipimo”, kinachoonesha kama Mjumbe huyo anafundisha au hafundishi kweli.
(Taurati) Isaya 8:20 “Na waende kwa Sheria na Ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na Neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.”

Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software v2.913

Maandiko ya Biblia yanatoka katika Toleo la King James (KJV)

Kwa maelezo zaidi: www.salahallah.com

Kitabu cha Mwenyezi Mungu

Sura 5:44
Al Maidah

Mfululizo na. 08