Kiswahili 17. “Je! hivi wanaweza kusikia wale waliozikwa kaburini”?

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

 

Nawasalimu katika jina lake Mwenyezi Mungu, mwenye rehema na huruma nyingi sana, baraka zake na ziwafunikeni leo hii! Rehema zake na ziwafikieni ninyi.
Somo letu linalovutia sana leo ni mojawapo ambalo wengi wana utata nalo. Hata miongoni mwa waumini, jambo hili halieleweki wazi kwa wengi sana. ‘Wafu wako wapi wanapoingia kaburini’ na ‘hivi je! naweza kuongea nao’? Wengi wanazo hisia kutokana na mafundisho waliyopokea kwa mababu zao kwamba mtu afapo anaendelea kuishi katika hali fulani ya ulimwengu wa ‘roho’. Kwamba bado yeye anaweza kuendelea kuongea na wapendwa wake. Somo hili juu ya kile kinachotokea mtu anapokufa ni la maana sana. Kwa maana ni jambo la maana mno kwamba sisi tuijue kweli hii. Ibilisi (Shetani) anajua fika ya kwamba kama sisi tumechanganyikiwa na hatuna hakika juu ya jambo hili, basi yeye anaweza kutupotosha na tena atatupotosha. Mara kwa mara Ibilisi atakuja hata kwa waumini na kuwafanya wafikiri kwamba bado wanaweza kuongea na wale waliokufa na kuingia makaburini mwao! Ataweza hata kuja katika umbile la wapendwa waliokufa na kusema maneno fulani yahusuyo maisha yetu binafsi. Hivyo wengi wanashawishiwa kuamini kwamba kwa vile mengi yanajulikana kwa hao wanaodhaniwa kuwa ni wale waliokufa, basi ni lazima mambo hayo yawe ya kweli. Kwa njia hii mamilioni wanadanganywa na kufikiri kwamba wafu hawajafa kabisa, bali wamo katika hali nyingine ya maisha. Haya yote ni kama Shetani (Ibilisi) anavyotaka yawe. Kwa njia hiyo anaweza kuwadanganya watu wengi sana wa dunia hii kwa kuwaambia uongo, yaani, uongo ambao kama utasikilizwa and kuzingatiwa utawaongoza watu kwenda kwenye maangamizi yao ya milele.
Uongo wa Kwanza…
Uongo wa kwanza uliowahi kusemwa duniani humu ulikuwa katika ile bustani nzuri ya Edeni. Wakati Ibilisi, kupitia ndani ya yule nyoka, aliposema na Hawa, mwanamke yule wa kwanza. Alimwambia uongo. Kabla ya hapo, Mwenyezi Mungu alikuwa amemweleza Hawa waziwazi na kwa mkazo kwamba yeye wala mumewe hawakupaswa kula matunda ya mti ule mmoja “uliokatazwa ambao ulikuwa katikati ya ile bustani”. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyonena nao na kuwaonya kwamba endapo wangeihalifu amri hii basi wangekufa. “Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Taurati Mwanzo 2:17.
Ibilisi, akimtumia yule nyoka kama chombo chake, alisema na kukana yale Mwenyezi Mungu aliyokuwa ameyaeleza wazi, “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa” Taurati Mwanzo 3:4
Majibu yapatikana wapi?
Tangu wakati ule wengi mno wameuamini uongo huo wa Ibilisi. Ibilisi ni baba wa uongo, kwa hiyo tusitazamie kitu cho chote kwake zaidi ya huo uongo. Leo tunataka kufanya utafiti wa vile Vitabu Vitakatifu Taurati na Injili ili kupata majibu kwa jambo hili la maana sana ambalo linaleteleza matokeo yatakayotuathiri milele. Ukweli wa Mwenyezi Mungu ni upi kuhusiana na wafu, na je! bado tunaweza kuendelea kuongea nao? Ili kupata hekima tunamtafuta Mwenyezi Mungu na njia yake. Yeye daima atawajulisha wale wanaonyenyekea chini ya mapenzi yake. Atawafunulia kweli yake wale wanaotaka kwa dhati kujua yaliyo sahihi na ya kweli. Daima twahitaji kutoa dua yetu kwa dhati kabla ya kuanza utafiti wetu.
Mwenyezi Mungu ameviteremsha Vitabu Vitakatifu kwa ajili yetu ili tujifunze tupate kuielewa ile kweli. Kumbukeni kile Mstahiki Nabii Muhammad alichokifunua katika Kurani Tukufu kwamba Taurati iliyoteremshwa kwa Musa na Injili iliyoteremshwa kwa Masihi Isa (Kristo Masihi) vilikuwa kwa mauidha yetu.
Hivyo yeye alisema vilikuwa kwa uongozi, nuru, na kupambanua baina ya yaliyo ya haki na yasiyokuwa ya haki.
Angalia:
Sura 2:53 Al Baqarah
Sura 3:3 Aali Imran
Sura 21:48 Al-Anbivaa
Ayubu mtumishi wa Mwenyezi Mungu!
Katika Sura 38:41 twaambiwa tu“mkumbuke mja wetu Ayubu”…Kwa nini Ayubu ni wa maana? Alikuwa mmojawapo wa watu wale wa Kale wa Mashariki aliyetembea na Mwenyezi Mungu. Alipita katika majaribu ya kusikitisha, lakini alidumu kumshikilia Mwenyezi Mungu hata alipojaribiwa vibaya sana na Ibilisi (Shetani). Ayubu mtumishi wa Mwenyezi Mungu alikuwa nayo mengi ya kusema kuhusu wafu. Anatupa sisi mauidha yanayofaa sana siku hizi ambayo tunayahitaji ili kuzikwepa hila zake Ibilisi. Kwa maana Ibilisi anatafuta kuwadanganya wengi, hata na ulimwengu mzima. Je, hivi tutayazingatia mauidha matakatifu aliyotupa mtumishi huyu mkuu wa Mwenyezi Mungu wa nyakati zile za Kale? Je, hivi maarifa aliyopewa hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu? Basi ni juu yetu sisi kuyatii mauidha hayo na kwa unyenyekevu kuwa miongoni mwa wanaojifunza.
Je, wafu wanaweza kuongea na walio hai? Ayubu ni mmojawapo tu wa waandishi wengi wa kile Kitabu Kitakatifu, ambaye atatupa sisi majibu. Hii hapa ni hekima itokayo katika Taurati Ayubu 14:7-14 ‘Kwani yako matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena, wala machipukizi yake hayatakoma. Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, na shina lake kufa katika udongo; Lakini kwa harufu ya maji utachipuka, na kutoa matawi kama mche. Lakini mwanadamu hufa, huifariki dunia; Naam, mwanadamu hutoa roho, naye yupo wapi? Kama vile maji kupwa katika bahari, na mto kupunguka na kukatika; ni vivyo mwanadamu hulala chini asiinuke; hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka, wala kuamshwa usingizini. Laiti ungenificha kuzimuni, ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita, na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka! Mtu akifa, je! atakuwa hai tena? Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.”
Ayubu mtumishi wa Mwenyezi Mungu anatuhakikishia kwamba baada ya mtu kufa hataamka, mpaka wakati wa ufufuo. Analala kaburini na Mwenyezi Mungu ataweka wakati ambapo badiliko hilo litatokea. Badiliko hilo linahusu ufufuo, wakati ule Masihi Isa arudipo kuwaita waaminifu wa Mwenyezi Mungu ili wawe hai tena na kuwachukua kwenda nao paradiso ya mbinguni.
Ibilisi asichotaka wewe ujue!
Kwa nini somo hili ni la muhimu mno kulielewa? Ibilisi anataka watu waamini kwamba wanapokufa hawafi kabisa, bali wanaendelea kuishi mahali fulani. Huo ni udanganyifu ambao kwa huo mamilioni wanadanganywa. Lakini ukweli ni kwamba…
‘Mtu afapo, analazwa mahali pa kupumzikia kaburini, wala hana kabisa sehemu yo yote ya kufanya katika jambo lo lote litendekalo hapa duniani’. Zingatia maneno haya ya Taurati: Mhubiri 9:5-6 “Kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua.”
Ibilisi anazichukia aya hizi zitokazo katika Taurati kwa kuwa hawezi kuwadanganya wale wanaoielewa kweli hiyo. Ibilisi atakuja katika umbile lile lile la wapendwa wetu wale waliokufa, akiwa na kisa kilicho tofauti sana na kile tunachoendelea kujifunza hapa. Ni wakati ule tu tunapolindwa na kuongozwa na Vitabu hivyo Vitakatifu na kwa njia ya Roho [Ruh] wa Mwenyezi Mungu twaweza kusimama na kuyapinga madanganyo ya Ibilisi katika siku hizi za mwisho.
Yeye (Ibilisi) atatuambia sisi kwamba wafu wanaweza kuongea na mwanadamu, na uongo mwingi unasemwa kwa watu na mara nyingi mno uongo huo unapokewa kama ndiyo kweli yenyewe.

035.022 “Wala hawawi sawa walio hai na wafu. Kwa yakini Mwenyezi Mungu Humsikilizisha Amtakaye; na wewe huwezi kuwasikilizisha waliomo makaburini. (Na hao kama wamekufa, wamo makaburini). Fatir 35:22
Je, Mstahiki Nabii Muhammad hakusema wazi juu ya jambo hili. Wale waliozikwa makaburini mwao hawawezi kusikia! Maisha yao yamekoma mpaka siku ya ufufuo. Hawana la ziada la kufanya tena katika jambo lo lote linalofanyika chini ya jua.
Masihi Isa alifundisha jambo lilo hilo, kwamba mtu anapokufa anaendelea kulala usingizi wa mauti mpaka hapo atakapoamshwa katika ufufuo. “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake” [Mwenyezi Mungu]. Injili Yohana 5:28. Hivi wako wapi anapowaita Masihi Isa? Inaeleza waziwazi kuwa wamo makaburini mwao. Mpendwa, rafiki yake Mwenyezi Mungu, unapozikubali kweli za Neno la Mwenyezi Mungu utaelewa na kuwa na amani kuhusu wale wanaoingia makaburini. Sasa wao wanangoja Uumbaji Mara ya Pili au kufufuliwa kwa wafu ambako kunatokea anaporudi Masihi Isa.

053.047 “Na kwamba ni juu Yake ufufuo mwingine” (Uumbaji wa Pili); An-Najm
Je, Uumbaji huo wa Pili unatokea lini? Katika Injili twaambiwa kwamba… “Kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda Italia, wa wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.” Injili 1 Wakorintho 15:52. Unatokea parapanda ya Mwenyezi Mungu inapolia. Huna haja ya kuwa na wasiwasi kuwa utaikosa kwa maana utaisikia kwa hakika parapanda ile. Mwenyezi Mungu atahakikisha kwamba hakuna atakayekosa kuisikia katika tukio hili la ulimwengu mzima. Kwa huzuni leo wengi huenda mahali pale ambapo wafu wanadhaniwa kuwa wanapandishwa juu kwa ajili ya kutoa mauidha yao. Zamani watu wa Mwenyezi Mungu walikatazwa kwenda kuangalia mambo kama hayo. “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” Taurati Mambo ya Walawi 19:31. Kitendo kama hiki ni kufanya mawasiliano na Mapepo (Majini) yanayojigeuza na kufanana kabisa na wale waliokufa. Mwenyezi Mungu amekataza sana kufanya jaribio lo lote kama hilo la kuongea na waliokufa. Yule adui aliyeanguka, Ibilisi husimama akiwa tayari kuwadanganya wote ambao hawatajali maagizo yaliyotolewa kwa makini ambayo yaliteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Leo hii Mwenyezi Mungu na akupe Amani yake ya Milele.
Aya zimenukuliwa kutoka DivineIslam’s Qur’an Viewer software
v2.913
Aya za Biblia zatoka katika Toleo la King James (KJV)
Wasiliana na: www.salahallah.com

“Je! hivi wanaweza kusikia wale waliozikwa kaburini?”
Sura 35:22
Fatir
Rudolf Martyn
_Mfululizo_Na.__17_