Kiswahili 36A. “Saa ya Hukumu”

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!
Wengi sana wamesikia na wanajua habari ya siku ile kuu ya Hukumu. Ni mara ngapi Maimamu wamejadiliana juu ya somo hili na kulisimulia kutoka katika Kurani Tukufu! Ni lini siku hiyo itakuwa imekaribia, je! sisi twaweza kujua? Je, tunajiandaaje kwa siku hiyo ya Hukumu? Je, twaweza kwa njia yo yote ile kuikwepa hiyo hukumu ya mwisho itakapokatwa na mahakama ile?

 

Wapendwa rafiki zake Mwenyezi Mungu, haya ni maswali machache tu tunayotarajia kuyajadili katika kipeperushi hiki. Mwenyezi Mungu na atupe neema, hekima, na amani ili tupate kulifahamu somo hili. Kurani Tukufu kwa wazi inasema juu ya Saa ya Hukumu.
“Na kwa kweli (Yeye Nabii Isa) ni alama ya Kiama (kuwa kinaanza kutukaribia); msikifanyie shaka na nifuateni. Hii ndiyo njia iliyonyoka.”
Sura 43:61 Az-Zukhruf
Awamu ya Upelelezi ya Hukumu
Kile ambacho watu wachache mno wanatambua ni kwamba kuna awamu ya upelelezi ya hiyo Hukumu Kuu. Kile ambacho wengi sana watakiona kuwa ni cha kushitua mno ni kwamba awamu hiyo ya upelelezi tayari imekwisha anza kwa watu wa dunia hii. Unabii wa zamani uliosahaulika katika Biblia unatuonya mapema ya kwamba siku hiyo tayari imekuja. Iko nyuma yetu zaidi ya vile tunavyodhani sisi kwa sayari hii dunia!

Je, awamu ya upelelezi ya Hukumu hii Kuu ni nini? Katika mahakama yo yote ya kidunia, mtu fulani anaposhitakiwa kuwa ametenda uhalifu fulani, muda unakuwapo mahakama inapokaa, na ushahidi unapoangaliwa kwa makini na kuchunguzwa na mahakama hiyo. Katika hukumu yo yote ya haki kuna kipindi hicho cha upelelezi wa uhalifu uliofanywa, mashahidi huitwa na kuhojiwa na kila jambo huangaliwa kwa makini kabla hukumu ya mwisho haijasomwa na hakimu. Katika kipindi hicho, mahakama inapitia matendo ya mshitakiwa. Jitihada zinafanywa kuona kuwa mambo yote yamekaguliwa kwa makini na kuchunguzwa, ili kujaribu kuona ni makusudi gani yaliyomsukuma mtu huyo kufanya yale aliyofanya.

Katika saa hii tuliyo nayo hivi sasa hapa duniani tumefikia katikati ya sehemu kubwa sana ya hukumu hiyo ya upelelezi inayoendelea. Hii ni kwa kiwango ambacho hakuna cho chote hapa duniani kiwezacho kulinganishwa nayo. Mmojawapo wa unabii wa Biblia wa kipindi kirefu sana katika Danieli 8:14 unatueleza kuhusu tukio hili. Unabii huo ulifikia mwisho wake mwaka 1844, nao wasema “ndipo patakatifu patakapotakaswa”. Unabii huo unaitwa “unabii wa miaka/siku 2300”.
“Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.” Danieli 8:14
Ni patakatifu gani ambapo Nabii Danieli anaongelea habari zake? Patakatifu hapo au hema hiyo takatifu ni lazima iwe mbinguni. Biblia inazungumza juu ya patakatifu au hema takatifu halisi za aina tatu, ya kwanza iliyotajwa ilikuwa katika siku zile za Musa.
Nabii Musa alikuwa amejenga mfano halisi wa patakatifu pale ambapo alikuwa amepaona akiwa juu ya Mlima pamoja na Mungu. Mfano huo halisi ulijengwa kule nje jangwani baada ya watoto wa Mungu kuondoka Misri. Patakatifu hapo pa jangwani palikuwa mfano halisi mdogo wa pale pa Mbinguni. Kitu fulani ambacho sisi tungeweza kufanya kwa ajili ya watoto wetu, ni kutengeneza mfano halisi wa ndege ambao ungefanana na ndege kubwa.

Musa akiwa juu ya vilele vile virefu vya Mlima Sinai alioneshwa picha ya Patakatifu pa Mbinguni au Hema Takatifu. Kisha aliagizwa na Mungu kujenga mfano halisi mdogo sawa na ule aliokuwa ameoneshwa. Alishauriwa hivi na Mungu…”Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, uliooneshwa mlimani.” Taurati Kutoka 25:40

Neno hilo ‘uvifanye’ lilijumuisha Patakatifu pamoja na vitu vyote vinavyohusu samani iliyomo ndani yake. Hivyo vyote vilifunuliwa kwa Musa akiwa juu ya Mlima Sinai.
Kurani Tukufu inalitaja tukio hilo katika aya hii ifuatayo.
“Na (kumbukeni khabari hii kadhalika:) Tulipochukua ahadi yenu (tukakwambieni): ‘Kamateni kwa nguvu haya tuliyokupeni na sikilizeni [sheria].’” Sura 2:93 Al Baqarah
Ni jambo la maana sana kwamba tujifunze somo hili kwa kuwa linafunua jinsi mchakato wa wokovu unavyotekelezwa Mbinguni. Linatupa picha ndogo sana ya kile kinachoendelea kule Mbinguni. Kwa hiyo sisi twaweza kujua ni wakati gani inaanza awamu ya hukumu hiyo ya upelelezi. Unabii wa siku/miaka 2300 ulipokwisha mwaka 1844, Hukumu Kuu ya Upelelezi ilianza kule Mbinguni. Hii ndiyo maana ya kufika muda wa kupatakasa Patakatifu. Patakatifu palipotajwa hapo katika Danieli ni lazima pawe Patakatifu pa Mbinguni, kwa maana patakatifu pale pa jangwani palipojengwa na Musa hatunapo tena na baadaye pakabadilishwa kwa mfano mkubwa zaidi uliojengwa na Sulemani, Mwanawe Daudi. Lakini patakatifu hapo pia hatunapo tena, na paliharibiwa mara mbili. Patakatifu na kutakaswa kwake ambapo pamenenwa katika Danieli ni lazima pawe ni pale pa Mbinguni ambako kiti cha enzi cha Mungu kiko na ambako mahakama inakaa.
“Kiti cha enzi cha utukufu, kilichowekwa juu tangu mwanzo, ndicho mahali patakatifu petu.” Yeremia 17:12. Ni kwa Patakatifu hapo ambapo tunapaswa kutazama kwa utimilifu wa Danieli 8:14.

Pia inataja kwamba patakatifu hapo au hema hiyo takatifu, ya kuwa haikujengwa kwa mikono ya mwanadamu… Injili Waebrania 8:2 “[Isa] Mhudumu wa patakatifu na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu.”
Mwombezi Wetu
Kumbukumbu za wanadamu wote duniani na za matendo yao yote yakiwa mema au mabaya, zimekusanywa na kuwekwa katika Patakatifu pale kule juu. Mahakama inakaa na kupitia maisha yetu na maamuzi hufanywa.

Katika kikao hicho cha mbinguni, Masihi Isa ndiye Mwombezi au Mpatanishi pekee kwa ajili yetu.
“Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu.”
Injili 1 Timotheo 2:5

Ni yeye peke yake anayestahiki kuwa mwombezi wetu, kwa kuwa ni yeye pekee aliyepata haki ya kufanya hivyo kwa kutwaa ubinadamu wetu alipokuja hapa duniani. Yeye bila ubinafsi wo wote alitoa maisha yake juu ya Mlima Moria, ambapo leo hii ipo “Kuba ya Mwamba” au “Msikiti Sharifu” kama kumbukumbu ya daima ya tukio lile la muda mrefu. Hapa pia mapokeo hutuambia kwamba ni mahali pale pale kabisa ambapo Ibrahimu aliitwa na Mungu kumtoa mwanawe kuwa sadaka.
Basi, katika Patakatifu pa Mbinguni Masihi Isa anadai damu yake mwenyewe kuwa inatosha kutukinga. Ni wakati huu wa sasa ambapo sisi hatuna budi kuzingatia hasa kile kinachoendelea kule. Ni wakati huu wa sasa wakati upelelezi huo unapoendelea yatupasa sisi kutafakari kwa makini yale yote ambayo Mungu kwa huruma yake ametufunulia. Wakati umewadia ambao Mungu anafanya mambo haya yajulikane ulimwenguni kote.

Wewe mpendwa msomaji unapendwa sana na Mwenyezi Mungu, upendo wake kwako unapita upendo uwao wote wa kibinadamu. Anakupenda wewe kwa upendo usio na kikomo na kwa shauku kubwa anatamani sana kuiokoa roho yako isiangamizwe milele. Hili ndilo kusudi la kwanza la kipeperushi hiki. Kuna nuru zaidi itakayofunuliwa kwa watu wake Mwenyezi Mungu. Yatupasa kuomba sana tupate kufunuliwa kweli hizi ambazo kwa muda mrefu zimefichwa kwa watu wengi. Leo usikiapo sauti yake ikisema nawe, itika kwake ukisema ndiyo! Kwa bidii mwombe Mwenyezi Mungu katika dua yako ya faragha akufunulie kweli hizi ambazo ni za muhimu kwako kuzijua kwa wakati huu wa Hukumu ya Upelelezi.
Hukumu Yote Amekabidhiwa Mwana
Siyo tu kwamba Isa ni mwombezi, bali twahitaji kufahamu ya kwamba Masihi Isa ndiye aliyeteremshwa kutoka Mbinguni kuwakomboa wote waliomo humu duniani. “[Isa] ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote…”
1 Timotheo 2:6
Ni Masihi Isa yuyu huyu ambaye ameaminiwa na kupewa hukumu ya mwisho ya watu wote.
“Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba liyempeleka.” Injili Yohana 5:22-23

Ni yale maamuzi ya mwisho, yaliyojengwa juu ya kumbukumbu zilizoko kule mbinguni zihusuzo chaguo letu tulilofanya upande wake au kinyume cha Mungu na kinyume cha yule aliyemteremsha hapa chini kwa ajili yetu, hilo ndilo litaamua matokeo ya hukumu ile itakavyokatwa. Ama tutapewa Uzima wa Milele, ama Mauti ya Milele. Hayo ndiyo malipo yatokanayo na hiyo hukumu. Kipindi hiki tunachoishi sisi ni kipindi cha kuogofya mno. Kingetufanya tupeleke dua zetu za dhati ili tupate kuonekana kuwa hatuna makosa siku ile majina yetu yatakapofikiriwa pale.
Kesi za wote waliomo humu duniani zinaletwa kwenye mahakama ile ya Mbinguni na wote wanachunguzwa kwa karibu sana kana kwamba hawakuwako watu wengine duniani ila wewe tu. Hivyo ndivyo ikatwavyo kwa karibu sana kila kesi.

Masihi Isa na Mahakama ile wanapomaliza kesi hizo, ndipo yeye anakuja duniani akiwa na ujira wake kwa ajili ya Wenye Haki. Waandishi wa kale wa Taurati walitabiri mapema tukio hilo, yaani, wakati atakaporudi na kuja na ujira wake.

“Tazameni,Bwana Mungu atakuja… Tazameni thawabu yake i pamoja naye…”” Taurati Isaya 40:10

Wazo lilo hilo limedhihirishwa katika Ufunuo wa Masihi Isa. Unatabiri waziwazi juu ya wakati ule Isa arudipo kwa ajili ya watu wake waaminifu waliomo duniani, naye analeta thawabu [zawadi] kwa kila mtu aliye mwaminifu.

“Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” Injili Ufunuo 22:12

Arudipo, kesi za wote zitakuwa zimekwisha katwa. Kwa maana, yeye angewezaje kuja na ujira kama hukumu hiyo ingekuwa bado iko mbele? Rafiki zangu, tunaishi katika Saa Kuu ya Hukumu. Isa arudipo katika mawingu ya Mbinguni, anakuja na ujira wa mwisho. Uzima wa Milele kwa waaminifu na wale wengine wanaangamizwa kwa mng’ao wa kuja kwake.
Tangazo la “Saa ya Hukumu ya Mungu” lilitolewa waziwazi katika miaka ile ya 1843-1844, wakati ujumbe wa pekee wa Ufunuo 14:6 ulipotangazwa waziwazi.

Leo wewe waweza kuwa tayari kwa tukio lile. Tuna Msaidizi wa Mbinguni katika hukumu hii, Masihi Isa; ndiye Mwombezi wako, mlilie yeye.

Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea (tovuti):
www.salahallah.com

Isa atakuwa ishara ya kuja kwa…
“Saa ya Hukumu”

Sura 43:61
Az-Zukhruf
Sehemu ya Kwanza

Mfululizo na.36 A